Mbunge awasilisha ombi la kuondolewa kwa jaji Maraga Kenya

Jaji mkuu David Maraga
Maelezo ya picha,

Jaji mkuu David Maraga

Mbunge wa chama tawala cha Jubilee nchini Kenya amewasilisha ombi la kutaka kufutwa kazi kwa jaji mkuu David Maraga.

Mbunge huyo wa Nyeri, Njiri Wambugu amewasilisha ombi lake mbele ya tume ya huduma za majaji akidai kwamba jaji Maraga alihusika katika kufanya makosa.

Akihutubia vyombo vya habari, mbunge huyo anadai kwamba Jaji huyo ''aliwashinikiza'' wenzake kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais Uhuu Kenyatta wakati alipotoa uamuzi wa kihistoria mnamo tarehe 1 Septemba.

Wambugu amefananisha ubatilishwaji wa matokeo hayo ya urais na mapinduzi ya majaji na sasa anataka nia ya jaji Maraga kuchunguzwa.

Wabunge wa chama cha Jubilee na rais Uhuru Kenyatta wamekuwa wakiukosoa uamuzi wa kufutilia mbali uchaguzi huo na wameendelea na kuwataja majaji hao kuwa ''wakora''.

Naibu wa rais William Ruto amesema kuwa baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa urais wa Oktoba 17, uamuzi huo wa majaji na sababu zao utaangaziwa upya.