Mwanafunzi wa sekondari apatikana akiwa na bunduki shuleni Kenya

Mwanafunzi wa sekondari apatikana akiwa na bunduki shuleni Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanafunzi wa sekondari apatikana akiwa na bunduki shuleni Kenya

Mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari katika kaunti ya Homabay nchini Kenya, anashikiliwa na polisi akitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kupatikana akiwa na bunduki, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation.

Mwanafunzi huyo wa umri wa miaka 17 alikamatwa siku ya Jumanne baada ya wanafunzi wawili kuripoti kuwa amekuwa akiwatisha kwa bunduki hiyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Dickens Bula, alisema kuwa usimamizi wa shule ulijulishwa na wanafunzi waliodai kuwa mwenzao amekuwa akiwatisha kuwa angewapiga risasi.

Gezeti hilo linasema kuwa baada ya mwanafunzi huyo kukamatwa na kuhojiwa, aliwapeleka polisi kwa kichaka kilichokuwa karibu ambapo alikuwa ameificha bunduki hiyo.

Daily Nation linasema kuwa bunduki hiyo ni ya kimarekani na hajaruhusiwa kutumiwa nchini Kenya.

Linasema kuwa licha ya uchunguzi kugundua kuwa bunduki hiyo haikuwa na risasi, usimamizi wa shule na wanafunzi walishikwa na hofu, na kusababsisha wanafunzi zaidi kuhojiwa kuhusu silaha hiyo.

Mkuu wa polisi eneo hilo Esau Ochorokodi, alisema mwanafunzi huyo aliwaambia wachunguzi kuwa alipata bunduki hiyo kutoka kwa jamaa wake anayeishi nchini Marekani.

Sasa mwanafunzi huyo anasubiri kushtakiwa kwa kumiliki bunduki bila kibali katika hakama ya Homa Bay.