Watu Wote: Filamu ya Kenya yashinda tuzo ya Oscars

Picha kutoka kwa filamu

Chanzo cha picha, TOBIAS ROSEN

Filamu kuhusu shambulizi la kigaidi la al-Shabab nchini Kenya ambapo watu 2 waliuawa ndani ya basi eneo la Mandera mwaka 2015 imeshinda tuzo la Oscars kitengo cha wanafunzi.

Filamu hiyo pia itawania tuzo kuu za Oscars kitengo cha filamu fupi mwaka ujao.

Ni filamu ya kwanza kutoka Kenya kushinda tuzo hiyo.

Filamu hiyo inayoeleza hadithi ya Kenya, kuhusu Wakenya na inashirikisha waigizaji wa Kenya, inasimulia shambulio hilo la mwaka 2014 kaskazini mwa Kenya, ambapo maudhui ya uadui wa kidini kati ya wakristo na waislamu yanaangaziwa.

Tuzo hiyo itatolewa tarehe 12 Oktoba, katika ukumbi wa Samuel Goldwyn Theater, Beverly Hills, Los Angales Marekani.

Ni mara ya kwanza ambapo filamu ya kenya imeteuliwa kuwania tuzo ya Oscars.

"Kenya sasa imepanda ngazi. Tunaongoza katika kueleza ulimwengu hadithi za Afrika," Matrid Nyaga, mwandaaji wa filamu hiyo ameambia BBC.

Katika shambulizi hilo, Waiwslamu walikataa kujitenga na Wakristo walipoamriwa kufanya hivyo na magaidi wa Alshabaab kutoka Somalia.

Chanzo cha picha, TOBIAS ROSEN

"Ni hadithi kuhusu Kenya na undugu wa Wakenya, na inaonyesha njia mwafaka ya kukabiliana na ugaidi kote Ulimwenguni"

Filamu hiyo iliyoundwa kwa ushirikiano wa wanafunzi wa Ujerumani na watengenezaji filamu wa Kenya inalenga kuwakumbuka mashujaa wa shambulizi hilo.

"Nina furaha kubwa! Cha kufurahisha ni kwamba filamu hii imetengenezwa kwa ushirikiano wa Wakenya. Sisi wote tulishirikiana kufanikisha ndoto hii" Tobias Rosen, mwandaaji wa filamu hiyo kutoka Ujerumani ameambia BBC.

Filamu itaonyeshwa Kenya kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Kwa kipindi cha Zaidi ya miongo miwili, Kenya imekuwa ikishambuliwa na magaidi wa Alshabaab.

Mwaka 2015, wanafunzi zaidi ya 147 waliuwawa na Alshabaab katika chuo kikuu cha Garissa kaskazini mwa Kenya.