Wanawake 100: ‘Sikukusudia kuyakubali makosa mahakamani'

Guard hands certificate to an inmate

Chanzo cha picha, AdvocAid

Miriam anaishi Sierra Leone na hakupata fursa ya kwenda shule.

Akiwa mtu mzima alikuwa na tatizo kusoma na kuandika na mwishowe alifungwa jela katika gereza la wanawake la Freetown.

Ni hapo ndipo alipata nafasi ya kuingia darasani kwa mara ya kwanza.

Miriam, ambaye hataki kutumia jina lake halisi amesaidiwa kuandika hadithi yake ya kujifunza kusoma.

Anaelezea BBC katika makala maalum ya Wanawake 100.

"Unakubali mashtaka au unakataa?"

"Ati nini? Sielewi."

"Unakubali mashtaka? Tafadhali nijibu."

"Ndio bwana."

Mwaka mmoja baadaye, niliachiliwa huru kutoka jela hiyo ya Freetown, Sierra Leone. Kwa nini nilikuwa huko? Kwa sababu sikufahamu kukubali shtaka kulimaanisha nini na hakukuwa na mtu yeyote kunitafsiria.

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 35, nilikamatwa wakati wa msako katika mtaa wangu baada ya wizi kufanyika. Tulipofikishwa mahakamani nilikubali makosa bila kufahamau kwa sababu sikusoma.

Nilipoanza kutumikia kifungo niliamua kuchukua masomo yaliyokuwa yanatolewa mara mbili kwa wiki kwa wafungwa wanawake.

Wafungwa wale wengine walikuwa kama mimi na hawakuwa wamewahi kwenda shule.

Baada ya miezi michache nilikuwa nimejifunza kutia saini na jina langu mwenyewe na sikutumia kidole cha gumba na wino kutia saini kwenye stakabadhi. Nilipenda masomo sana hadi wanawake walee wengine wakanipa jina la Msichana wa shule.

Tangu nilipoachiliwa nimeanzisha biashara yangu inayokimu mahitaji ya familia yangu.

Kwa sababu ya ujuzi wangu mpya, sasa mimi ni mwenyekiti wa wanawake wa soko, na ninaweza kuweka rekodi zote za kifedha kwa vizuri.

Wakati sina kazi sokoni, mimi huwafunza watoto mtaani kusoma na kuandika kutumia mbinu nilizosoma nilipokuwa mfungwa.

Vyeti vyangu vya elimu ni thibitisho kuwa ninaweza kusoma, kuandika na kufanya hesabu. Ni mojawapo ya mafanikio yangu ambayo ninayojivunia sana .

Bado ninahitaji msaada kuandika nakala hii, lakini ukinisaidia ninajua kile ninachotaka kukuambia kimeandikwa kwenye karatasi na hii inanifanya nihisi niko kwenye usukani, hisia ambayo sijawahi kuwa nayo.

Wanawake 100 ni nini?

Katika Msimu wa Wanawake 100 wa BBC, huwa tunawataja wanawake 100 wenye ushawishi na wanaowahamasisha wengine kutoka kila pembe ya dunia kila mwaka. Mwaka 2017, tunatoa changamoto kwao kukabili matatizo manne makuu yanayokabili wanawake siku hizi - vikwazo katika kupanga ngazi katika jamii, kutojua kusoma na kuandika miongoni mwa wanawake, kudhalilishwa wakiwa maeneo ya umma na kunyanyaswa michezoni.

Kwa usaidizi wako, watatafuta suluhu kwa matatizo hayo na tunataka ushiriki kwa kutoa mawazo hayo. Tupate katika Facebook, Instagram na Twitter na utumie kitambulisha mada #Wanawake100

Chanzo cha picha, AdvocAid

Maelezo ya picha,

Wafungwa wakiwa na walimu darasani

Haja Gbla hufanya kazi kama mwalimu katika idara ya magereza, ambapo huwasaidia wanawake kupata elimu, kupitia mashirika la hisani ya charities EducAid na AdvocAid. Sawa na Miriam, hakupata elimu ya kawaida alipokuwa mtoto, lakini shirika hilo la hisani lilimpa fursa ya kurejea darasani na kumaliza masomo yake.

Katika magereza na vituo vya kurekebishia tabia, nimekutana na wanawake wengi sana ambao wana visa vya kushangaza vya kunyimwa haki.

Wengi walijipata taabani kwa sababu ya kukosa fursa ya kupata elimu.

Kuna wengi waliotia muhuri au saini nyaraka za kupigwa chapa ambazo hawakufahamu zilikuwa zinasema nini, wale ambao wameyakiri makosa bila kujua, na wengine ambao wamefungwa kwa kukiuka mikataba ya kifedha isiyo ya haki ambayo walitia saini kwa sababu hawakuwa wanafahamu inasema nini.

Kuendesha masomo gerezani kulinipa fursa ya kutambua jinsi walivyo na bahati wale ambao wana fursa ya kupata elimu na jinsi inavyoweza kuwa taabu mtu kukosa elimu.

Nimekuwa na nyakati nyingi za kujivunia, nikitazama wanawake wakibadilika baada ya kutambua kwamba wenyewe pia wanaweza kushika kalamu, waweze kusoma majina yao kwenye orodha fulani, wahesabu faida na gharama kwenye biashara zao, au wasome na kufurahia kitabu.

Inafurahisha sana hasa wanawake wanaposhangiliwa wanapohitimu kutoka darasa moja hadi jingine na kupokea vyeti na tuzo mbalimbali.

Chanzo cha picha, AdvocAid

Maelezo ya picha,

Wanafunzi katika jela hiyo hupewa vyetu vya ufanisi wanapopiga hatua

Katika kazi yangu ndani na nje ya jela, huwa najifahamu kwamba mimi ni kama kichocheo cha kuwawezesha wanawake kufikia uwezo wao kamili.

Elimu ni nyenzo muhimu ya kufungua milango na fursa na kubadilisha nafasi kwa mwanamke na kumuwezesha kuyadhibiti maisha yake mwenyewe.

Jinsi kupata kwangu elimu kupitia EducAid kulivyoniwezesha kufikia uwezo waku na kuwa ajenti wa mageuzi, ninataka wanawake wengine vijana niwasaidie kadiri niwezavyo wajiunge na 'jeshi' la wanawake ambao wanahitaji kuhakikisha kwamba kuna haki na usawa kwa wanawake Sierra Leone na kwingineko.

Ni jambo la kusikitisha kwamba mgogoro wa kisasa wa kiuchumi baada ya mlipuko wa Ebola wa hivi majuzi umesababisha kupunguzwa kwa pesa za ufadhili zinazotolewa kwa mashirika ya haki za kibinadamu.

Kwa sababu ya hili, madarasa ya kufunza watu kusoma na kuandika yamefungwa kwa muda kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10.

Wanawake walio gerezani wanataka madarasa haya yafunguliwe tena, na wanayatazama kama fursa ya kuimarisha nafasi zao za kuwa na maisha yenye ufanisi watakapoachiliwa kutoka gerezani.

Chanzo cha picha, AdvocAid

Maelezo ya picha,

Mashirika ya hisani hutoa vitabu vya kusomwa na wafungwa wakiwa gerezani

*Jina la Miriam limebadilishwa