''Wapenzi 20 wa jinsia moja'' wakamatwa Zanzibar

Wapenzi wa jinsia moja
Maelezo ya picha,

Wapenzi wa jinsia moja

Mamlaka ya kisiwani Zanzibar imewakamata watu 20 wanaotuhumiwa kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja, kisa hicho cha hivi karibu kikitokea wakati wa msako dhidi ya watu wa jinsia moja katika kisiwa hicho cha Afrika mashariki.

Wanawake 12 na wanaume 8 walikamatwa kufuatia uvamizi wa polisi katika hoteli moja ambapo washukiwa hao walikuwa wakishiriki katika warsha kulingana na afisa mkuu wa polisi Hassan Ali.

''Ni kweli tuliweza kuwakamata kwa sababu tunashuku kwamba walikuwa wakishiriki katika mapenzi ya jinsia moja kitu ambacho ni kinyume na sheria kisiwani zanzibar na ni ukiukaji wa wa sheria za taifa la Tanzania'', alisema akiongezea kuwa polisi wataongeza doria zao dhidi ya makundi kama hayo.

Mapenzi ya jinsia moja ni uhalifu nchini Tanzania na ngono miongoni mwa wanaume ni hatia inayovutia kifungo cha kati ya miaka 30 jela na kifungo cha maisha.

Mamlaka ya Tanzania hivi majuzi ilifanya msako dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, mnamo mwezi Septemba 2016 , serikali ilisitisha kwa muda miradi ya ukimwi ya wapenzi wa jinsia moja.

Mnamo mwezi Februari , serikali ilisitisha huduma za vituo 40 vya afya vya kibinafsi kwa madai kwamba vilikuwa vikitoa huduma kwa wapenzi wa jinsia moja.