BBC yazindua idhaa mpya za Pembe ya Afrika

Tovuti hizo mpya tayari zimeanza kuwavutia watu
Maelezo ya picha,

Tovuti hizo mpya tayari zimeanza kuwavutia watu

Idhaa ya Dunia ya BBC imezindua tovuti tatu mpya za habari ambazo zinalenga kuhudumia watu kutoka mataifa mawili ya Pembe ya Afrika - Ethiopia na Eritrea - kama sehemu ya upanuzi mkubwa zaidi wa idhaa hiyo tangu miaka ya 1940.

Tovuti hizo tatu zitakuwa "chanzo cha ukweli" katika eneo ambalo uhuru wa vyombo vya habari ni finyu, amesema mhariri wa BBC Will Ross.

Uzinduzi wa tovuti hizo za lugha za Amharic, Afaan Oromo na Tigrinya utafuatwa miezi michache ijayo na kuzinduliwa kwa matangazo ya redio kwa lugha hizo tatu.

Serikali ya Uingereza ilitangaza kutoa ufadhili mkubwa wa Idhaa ya Dunia mwaka 2015.

Hilo limesaidia kufanyika kwa upanuzi mkubwa Afrika na Asia.

"Tunafahamu kwamba kuna kiu sana miongoni mwa watu wa Ethiopia na Eritrea ya kupata habari mseto na za kiwango cha hali ya juu kwa lugha za Amharic, Afaan Oromo na Tigrinya," amesema Ross, mkuu wa idhaa hizo mpya.

Eritrea ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Ethiopia mwaka 1993 baada ya vita vilivyodumu miaka 30.

Uhasama kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuwepo na mpaka wa nchi hizo mbili huwa umefungwa na kuwekwa chini ya ulinzi mkali.

Inakadiriwa kwamba watu 80,000 walifariki vita vilipozuka kati ya nchi hizo mbili kutokana na mzozo wa mpakani mwaka 1998 hadi 2000.

Ross amesema anaamini kwamba kuna fursa kubwa ya kupata wasikilizaji katika nchi hizo mbili - ambazo kwa pamoja zina watu zaidi ya 100 milioni.

Amesema pia kwamba mitandao ya kijamii itachangia zaidi katika kuwapata wasomaji, watazamaji na wasikilizaji wa umri mdogo.

Jamhuri ya Ethiopia

Mji mkuu: Addis Ababa

 • Idadi ya watu 86.5 milioni

 • Ukubwa wa eneo Kilomita 1.13 milioni mraba (maili 437,794 milioni mraba)

 • Lugha kuu Amharic, Oromo, Tigrinya, Kisomali

 • Dini kuu Kikristo, Kiislamu

 • Umri wa watu kuishi Miaka 58 (wanaume), miaka 62 (wanawake)

 • Sarafu Birr

Getty Images

"Kuna pia idadi kubwa ya watu wa nchi hizo mbili wanaoishi nchi za nje, ambao wamesalia kuwa na uhusiano wa karibu sana na 'nyumbani'. Hali ya kisiasa katika nchi hizo mbili pia imechangia kuwepo kwa raia wanaoishi nje ya nchi ambao huwa wanaeleza hisia zao na kuendesha juhudi za uanaharakati," amesema.

"Kwa sasa, chanzo kikuu cha habari kwa wengi Ethiopia huwa ni vyombo ambavyo vinaunga mkono sana serikali ndani ya nchi hizo au vyombo vinavyoipinga sana serikali kutoka nje ya nchi."

Taifa la Eritrea

Mji mkuu: Asmara

 • Idadi ya watu 5.6 milioni

 • Ukubwa wa eneo Kilomita 117,400 mraba (maili 45,300 mraba)

 • Lugha kuu Tigrinya, Tigre, Kiarabu, Kiingereza

 • Dini kuu Kiislamu, Kikristo

 • Umri wa watu kuishi Miaka 60 (wanaume), miaka 64 (wanawake)

 • Sarafu Nakfa

Getty Images

Tayari kurasa za Facebook za idhaa hizo tatu zimewavutia watu sana mtandaoni.

Ukurasa wa Afaan Oromo ulikuwa umefuatwa na watu zaidi ya 30,000 siku tatu za kwanza baada ya kuzinduliwa.

Hata hivyo, kuenea kwa huduma ya mtandao ni kwa kiwango cha chini sana katika nchi hizo mbili, na kuzinduliwa kwa matangazo ya redio kutakuwa kiungo muhimu katika kutoa "habari mseto za kiwango cha juu" kwa Waethiopia na Waeritrea, amesema Ross.

"Lengo kuu la habari zetu litakuwa kuwasaidia Waethiopia na Waeritrea kufahamu vyema zaidi nafasi yao duniani. Idhaa hizo mpya pia zitasaidia wasikilizaji, wasomaji na watazamaji wa BBC kote duniani kuwa na ufahamu bora zaidi wa Pembe ya Afrika," ameongeza.

Idhaa za Afrika:

 • Afaan Oromo: Lugha inayozungumzwa na kabila kubwa zaidi Ethiopia
 • Amharic: Lugha rasmi ya Ethiopia
 • Tigrinya: Lugha kuu ya kufanyia kazi Eritrea, pamoja na Kiarabu. Pia huzungumzwa Ethiopia
 • Igbo: Lugha rasmi Nigeria. Pia huzungumzwa Equatorial Guinea
 • Yoruba: Huzungumzwa kusini magharibi mwa Nigeria na baadhi ya maeneo mengine ya Afrika Magharibi, sana Benin na Togo
 • Pidgin: Aina ya Kiingereza cha mtaani ambayo huzungumzwa kusini mwa Nigeria, Ghana, Cameroon na Equatorial Guinea

Idhaa za Asia:

 • Gujarati: Asili yake ni jimbo la Gujarat nchini India, lakini wazungumzaji wake hupatikana kote India na maeneo mengine duniani
 • Marathi: Kutoka jimbo la Maharashtra, nchini India, ambalo hujumuisha pia mji mkuu kibiashara wa Mumbai
 • Telugu: Huzungumzwa na watu wengi sana, sawa na lugha nyingine za India, zaidi majimbo ya Andhra Pradesh na Telangana
 • Punjabi: Moja ya lugha zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, huzungumzwa zaidi Pakistan na maeneo ya India
 • Korean: Huzungumzwa Kusini na Kaskazini ingawa kuna lahaja tofauti. Maneno mengi mapya kutokana na utamaduni wa Pop, na pia maneno ya kutoholewa kutoka lugha za nje hupatikana zaidi Kusini.