Makamanda wa jeshi la DRC waliwauwa mamia

Risasi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Majenerali waliotajwa katika ripoti wamekuwa wakikana kuwajibika kwao binafsi na mauaji hayo.

Makamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walipanga wimbi la mauaji ya kikatili ambapo mamia kadhaa ya watu waliuawa kati ya mwaka 2014-2016 kaskazini mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, limeripoti shirika la habari la Reuters.

Mashirika ya habari yananukuu taarifa hizi kutoka kwa kikundi cha utafiti nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CRG) kilichowahoji wahusika 249, mashahidi na waathiriwa

CRG ilielezea ushahidi wa watu kadhaa wakisema kwamba makamanda walisaidia na wakati mwingine kuandaa mauaji. Wakati wa baadhi ya mauaji hayo ya kinyama vyanzo vya habari vilikieleza kikundi cha CRG, kwamba askari waliweka vizuwizi ili kuwazuwia waathiriwa wasitoroke mauaji.

Ripoti inasema kuwa mauaji ya kwanza yalipangwa mnamo mwaka 2013 na kiongozi wa zamani wa Popular Congolese Army waliokuwa wakijaribu kuondoa imani kwa kikosi cha serikali kuu.

Msemaji wa serikali ya Kongo Lambert Mende amesema kuwa maafisa kadhaa wa vyeo vya juu nchini humo walihukumiwa kwa nafasi yao katika mauaji hayo, lakini akakikosoa kikundi cha CRG kwa "kujaribu kuibua mambo ya zamani ",limeeleza shirika la Reuters.

Majenerali waliotajwa katika ripoti wamekuwa wakikana kuwajibika kwao binafsi na mauaji hayo.