''Mwanasheria mkuu asema hakuna pengo la serikali ya mpito Kenya''

Mwanasheria mkuu nchini Kenya Githu Muigai Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Mwanasheria mkuu nchini Kenya Githu Muigai

Mwanasheria mkuu Kenya Githu Muigai amepuuzilia mbali madai kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa mzozo wa kikatiba wakati ambapo taifa hilo linajiandaa kufanya uchaguzi mpya .

Bwana Muigai siku ya Alhamisi alisema kuwa madai ya hivi majuzi ya mawakili wa upinzani kwamba serikali ya mpito itabuniwa iwapo tume ya uchaguzi itashindwa kufanya uchaguzi hayana ukweli.

Akizungumza katika afisi yake, mshauri huyo wa serikali amesema kuwa rais Uhuru Kenyatta ataendelea kushikilia mamlaka yote aliyopewa hadi pale rais mwengine atakapochaguliwa.

Mamlaka hayo alisema yatashirikisha yale ya kuwa kamanda mkuu wa jeshi .

Mawakili wa Nasa wakiongozwa na James Orengo wametaja mamlaka yanayoshikiliwa na rais Uhuru Kenyatta kuwa ya muda.

Kifungu hicho kinataja muda kati ya tarehe ya uchaguzi na siku ile ambayo rais mpya ataapishwa.

Muigai amesema kuwa katiba itamzuia rais Kenyatta kutekeleza majukumu kadhaa kama ilivyo katika kifungu cha 132-2.

''Majukumu hayo ni kuteua majaji, kuteua ama kufuta kazi mawaziri ama afisa yeyote wa serikali .Hakuna pengo la kuunda serikali yoyote ile, hadi siku ya kuapishwa kwa rais mpya, uongozi wa serikali hauwezi kubadilika'', alisema..

Wakenya wanatarajiwa kushiriki katika marudio ya uchaguzi mkuu wa urais ifikiapo tarehe 26 Oktoba baada ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8 kufutiliwa mbali na mahakama ya juu.