Sababu tano zinazozuia mageuzi kuhusu umiliki wa bunduki Marekani

Donald Trump holding a long gun

Baada ya mauaji ya watu 17 katika shule moja Florida 14 Februari, na mwaka jana kufuatia kuuawa kwa watu 59 jijini Las Vegas, Nevada watetezi wa udhibiti wa silaha nchini Marekani wameanza kuzidisha kampeni yao.

Ni kisa ambacho kinaonekana kuwa cha kawaida, kwani hilo hutokea kila baada ya mauaji kutekelezwa kwa kutumia bunduki.

Katika ngazi ya taifa, licha ya utafiti kuonyesha kwamba watu wengi wangependa kukazwa kwa sheria za kuwaruhusu watu kumiliki silaha, bado hakuna hatua iliyochukuliwa kutunga sheria kwa miongo kadha.

Miongoni mwa mambo ambayo hupendekezwa ni uchunguzi zaidi wa historia na maisha ya mtu kabla yake kuuziwa silaha.

Aidha, kupigwa marufuku kwa bunduki zenye uwezo mkubwa sawa na zile zinazotumiwa na jeshi.

Baada ya idadi kubwa ya watu kuuawa wakati huu, huenda shinikizo za kufanyika kwa mabadiliko zitazidi.

Hapa chini ni sababu nne ambazo zimezuia kufanyiwa mageuzi kwa sheria kuhusu silaha Marekani.

Kundi la NRA

Maelezo ya picha,

Mwanamke akiwa na bunduki maonesho ya NRA

Chama cha wamiliki wa bunduki Marekani (NRA) ni moja ya makundi yenye ushawishi mkubwa zaidi katika silaha za Marekani. Si kwa sababu tu kuwa hutumia pesa nyingi kupata uungwaji mkono wa wanasiasa, bali pia kwa sababu ya wanachama wake ambao wanakaribia milioni tano.

Chama hicho hupinga mapendekezo mengi ya kudhibiti silaha.

Ni chama hiki ambacho huongoza juhudi za kushinikiza serikali za taifa na za majimbo kuondoa baadhi ya masharti yanayodhibiti umiliki wwa silaha.

Mwaka 2016, NRA walitumia jumla ya $4m kupata uungwa mkono wa wanasiasa na pia kutoa michango kwa wanasiasa.

Aidha, chama hicho kilitumia zaidi ya $50m katika kampeni za kisiasa. Inakadiriwa kwamba walitumia $30m kusaidia kuchaguliwa kwa Donald Trump kuwa rais.

Bajeti ya jumla ya chama hicho ni karibu $250m.

Ni chama ambacho kinaweza kuwajenga au kuwaangamiza wanasiasa.

Hili linaweza kubadilika? Makundi ya kutetea udhibiti wa silaha, yakiungwa mkono na watu matajiri mfano meya wa zamani wa New York Michael Bloomberg, yamekuwa yakijiandaa kukabiliana na nguvu za NRA kisiasa. Lakini bado yana kibarua kigumu.

Mipaka ya maeneo

Juhudi nyingi za karibuni za kudhibiti zaidi silaha hushindwa hata kabla ya 'kuanza kabisa'. Huzuiwa katika Bunge la Wawakilishi, ambalo limedhibitiwa na chama cha Republican tangu 2011.

Juni mwaka 2016 kundi la wanasiasa wa Democratic lilisusia shughuli bungeni kulalamikia uamuzi wa viongozi wa Bunge hilo kutoitisha kura kuhusu miswada miwili ya udhibiti wa silaha.

Bunge hilo huonekana kuegemea upande wa watetezi wa haki za watu kumiliki silaha, sawa na lilivyoegemea chama cha Republican kwa wingi wa wabunge.

Maelezo ya picha,

Wabunge wa Democratic wakiwa wameketi sakafuni ndani ya Bunge kulalamikia ubabe wa chama cha Republican Juni mwaka jana

Kutokana na jinsi mipaka ya maeneo ya uwakilishi bungeni ilivyo, ambapo maeneo ya Republican hupata wabunge wengi, kuna viti vingi "salama" vya Republican kuliko vya Democratic.

Katika maeneo hayo ya bunge, wanasiasa mara nyingi hufuata matakwa ya wapiga kura wa msingi, ambao sana huongozwa na masuala ya msingi zaidi kwao mfano haki za kumiliki silaha.

Gharama ya kuwaudhi wapiga kura hawa huwa ya juu sana kisiasa kuliko ile ya kuwaudhi wanaotaka silaha zidhibitiwe.

Wengi wa wanaounga mkono kudhibitiwa kwa silaha isitoshe huwa hawapigi kura katika mchujo wa chama cha Republican kwani wengi si wanachama.

Idadi ya watu na maeneo wanamoishi pia huchangia. Kuna maeneo mengi ya uwakilishi maeneo ya mashinani yenye watu wengi wanaomiliki silaha kuliko maeneo ya mijini.

Kuongezeka kwa watu wanaotaka silaha zidhibitiwe wanaoishi miji huwa hakuchangii kubadilisha hali kwa jumla katika Bunge.

Hili linaweza kubadilika? Hili linaweza tu kubadilika iwapo watu wengi wenye mtazamo huria watahama kutoka mijini na kwenda maeneo ya mashambani. Njia nyingine ni kubadilisha mipaka maeneo kama ya Wisconsin ambapo Republican huwa na nafuu, lakini hilo haliwezi kufanyika kwa urahisi.

Kikwazo zaidi

Hata kama mswada wa kudhibiti silaha utapitishwa na Bunge la Wawakilishi, bado utahitaji kupitishwa na Bunge la Seneti ambapo mgawanyiko kati ya maeneo ya mashambani na ya mijini hujitokeza pia.

Majimbo yenye wakazi wengi wa mijini kama vile New York, Massachusetts au California huzidiwa na majimbo ya maeneo mengi ya mashambani na ya kusini mwa nchi hiyo ambayo huunga mkono kumilikuwa kwa silaha.

Sheria za seneti pia zinaweza kuzuia sheria zaidi za kudhibiti silaha kwa kutumia "kujivuta" ambapo wabunge au maseneta hutumia muda mwingi na hotuba ndefu kuchelewesha upitishwaji wa sheria. Hili huzuia mswada kupigia kura.

Hilo mara nyingi limechangia kuwepo kwa hitaji la mswada kupigiwa kura 60 kati ya 100 kwenye Seneti badala ya wingi wa jumla (kura 51).

Kupatikana kwa kura 60 ndiko pekee kunakoweza kuzuia kutumiwa kwa mbinu hiyo ya "kujivuta".

Mwaka 2013 baada ya mauaji katika shule moja Newtown, Connecticut kulikuwepo matumaini sheria ingepitishwa kushurutisha wauzaji wa silaha kuchunguza historia ya wanunuzi wa silaha. Baada ya kura kupigwa, mswada huo ulipata kura 56 pekee, na kupungukiwa na kura nne kukwepa mbinu hiyo ya "kujivuta".

Hakuna sheria ya kudhibiti silaha iliyowahi kupitishwa tangu wakati huo.

Hili linaweza kubadilika? Trump amekuwa miongoni mwa wanaopinga zaidi mbinu hiyo kwani imemzuia kupitishwa sheria anazotaka. Wengi wa maseneta hata hivyo wanapinga hilo.

Mahakama

Maelezo ya picha,

Waandamanaji nje ya Mahakama ya Juu mwaka 2008

Huku bunge la Congress likionekana kuangazia zaidi kuondoa sheria zilizopo sasa za kudhibiti silaha, majimbo yanayoegemea siasa za mrengo wa kushoto zimechukua jukumu muhimu katika kutekeleza mikakati ya kudhibiti siasa.

Baada ya mauaji ya wanafunzi shuleni Newtown, Connecticut, mwaka 2012, majimbi 21 yalipitisha sheria mpya za kudhibiti silaha, zikiwemo marufuku ya kumiliki bunduki zenye uwezo mkubwa Connecticut, Maryland na New York.

Baadhi ya sheria hizo zimekumbana na kikwazo kingine - Mahakama. Miaka ya karibuni, Mahakama ya Juu imetoa uamuzi mara mbili kwamba haki ya watu kumiliki silaha imo kwenye katiba.

Mwaka 2008, Mahakama ya Juu iliamua kwamba Marekebisho ya Pili kwenye katiba ya Marekani yalitoa haki wazi kwa watu kumiliki silaha na kwamba marekebisho hayo yanaharamisha juhudi zozote za kudhibiti kumilikiwa kwa silaha na watu binafsi.

Hili linaweza kubadilika? Jaji Neil Gorsuch ambaye alichaguliwa na Trump ameweka wazi msimamo wake kwamba anatazama Marekebisho ya Pili kwa uwazi. Rais huyo pia anajaza nafasi kwenye mahakama za chini na majaji ambao wanaunga mkono haki za watu kumiliki silaha.

Msisimko

Changamoto ngingine kitaifa ni kwamba wapinzani wa mageuzi hayo mara nyingi huwa hawabadili msimamo wao.

Uungwaji mkono wa mageuzi ya kisheria hata hivyo hukaa ukibadilika kila visa vipya vya mauaji ya kutumia silaha vinaporipotiwa.

Mkakati wa NRA, na wa wanasiasa wanaounga mkono haki za watu kumiliki silaha, ni kusubiri wimbi lipite. Kuchelewesha upitishwaji wa sheria hadi watu wasahau na waangazie mambo mengine.

Jumatatu, afisa anayehusika na wanahabari White House Sarah Huckabee Sanders aliwaambia wanahabari kwamba "kuna wakati na pahala pa mjadala wa kisiasa, lakini huu ni wakati wa kuungana kama taifa".

Maelezo ya picha,

Mwanamandaji nje ya kiwanda cha kuunda bunduki mwaka 2016

Trump alipokuwa akiondoka White House kwenda Puerto Rico, alisema "tutazungumzia sheria hizi za bunduki muda unavyosonga."

Kama ilivyo kwenye filamu ya Casablanca, muda unavyosonga, hadithi imekuwa ni ile ile.

Hili linaweza kubadilika? Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa wakati wa kampeni za urais mwaka 2016, suala la udhibiti wa umiliki wa bunduki lilikuwa muhimu kwa wafuasi wa Democratic na Republican.

Hiyo ilikuwa baada ya mauaji yaliyotekelezwa kilabu cha wapenzi wa jinsia moja Orlando. Hilo huenda lilichangia, au ulikuwa mwanzo mpya?