Raila Odinga ajiondoa kwenye uchaguzi Kenya

Raila Odinga ajiondoa kwenye uchaguzi mkuu Kenya Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raila Odinga ajiondoa kwenye uchaguzi mkuu Kenya

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ametangaza kuwa hatashiriki kwenye uchaguzi mkuu ambao unapangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu.

Bwana Odinga anasema anataka kufanyika uchaguzi mpya jinsi ilivyoamuliwa na mahakama ya juu

Uchaguzi huo wa tarehe 26 utakuwa ni marudio ya uchaguzi mkuu, baada ya mahakama ya juu nchini Kenya kufuta matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 mwezi Agosti mwaka huu.

Bw. Odinga anasema amejiondoa ili kuipa tume ya uchaguzi IEBC, muda wa kutosha kufanya mabadiliko ambayo yatawezesha kufanyika uchaguzi kwa njia iliyo nzuri.

Awali tume ya uchaguzi ilikuwa imemtangaza rais wa sasa Uhuru Kenyatta kuwa mshindi.

Ilisema kuwa Bw. Kenyatta alishinda uchaguzi huo kwa kura milioni 1.4.

Upinzani nchini Kenya awali ulikuwa umetangaza wazi kuwa ungeshiriki kwenye uchaguzi mkuu ikiwa mabadiliko yanayostahili yangefanyika.

Image caption Bwana Odinga anasema anataka kufanyika uchaguzi mpya jinsi ilivyoamuliwa na mahakama ya juu

Upinzani unaamini kuwa uchaguzi unastahili kufutwa baada ya Odinga kujiondoa, na kutoa muda wa kutosha kufanyika mabadiliko yanayostahili ili uchaguzi kufanyika kuambatana na sheria na katiba.

Serikali imekuwa ikisema kuwa uchaguzi utafanyika na rais kuapishwa.

Bw. Odinga pia ametoa wito kwa watu kuandamana kesho Jumatano kwa kutumia kauli mbiu "hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi".

Mwezi Septemba mwendesha mashtaka mkuu nchini Kenya Keriako Tobiko, aliamrisha polisi na tume ya kupambana na ufisadi kuchunguza ikiwa wanachama wa tume ya uchaguzi walihusika na uhalifu wowote.

Alitaka wachunguzi kuchunguza madai kuwa maafisa wawili wakuu wa upinzani walikuwa wamedukua mitandao ya tume ya uchaguzi.

Mada zinazohusiana