Wabunge Kenya waidhinisha marekebisho ya sheria za uchaguzi

Bunge la Kenya

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Bunge la Taifa nchini Kenya limepitisha mswada tata wa kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi.

Muungano wa upinzani umepinga vikali marekebisho hayo.

Chama tawala cha Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta kimekuwa kikiunga mkono marekebisho hayo ambayo kinasema yanahitajika kulainisha mfumo wa uchaguzi nchini humo baada ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti kufutwa na Mahakama ya Juu.

Bw Kenyatta alikuwa ameahidi kuidhinisha mswada huo kuwa sheria pindi ukipitishwa na Bunge.

Miongoni mwa mengine, wabunge wameidhinisha Tume ya Uchaguzi (IEBC) iruhusiwe kumtangaza mgombea atakayesalia baada ya mpinzani wake kujiuzulu uchaguzi wa marudio utakaotokana na kesi ya uchaguzi kuwa mshindi moja kwa moja.

Hatua hiyo imejiri siku moja baada ya mgombea wa upinzani Raila Odinga kujiondoa akisema mageuzi ambayo yanahitajika katika IEBC bado hayajatekelezwa.

Iwapo mswada huo ungekuwa sheria, Bw Kenyatta angetangazwa mshindi moja kwa moja.

Hata hivyo, uamuzi wa Mahakama ya Juu mwaka 2013 ulikuwa unatoa uwezekano wa uchaguzi mpya kuitishwa katika kipindi cha siku 90, jambo ambalo Bw Odinga amesema linafaa kufanyika.

Kwa sasa hata hivyo, mgombea mwingine Ekuru Aukot ameshinda kesi ya kutaka ajumuishwe kwenye uchaguzi huo uliopangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba, hivyo basi Bw Kenyatta hawezi kutangazwa mshindi moja kwa moja.

Mswada huo wa marekebisho aidha unataka tume ishurutishwe kuwasilisha matokeo ya uchaguzi kutoka vituoni kwa njia ya kielektroniki na kuwasilisha pia fomu za matokeo zenyewe hadi vituo vya kuhesabia kura katika ngazi ya eneo bunge na kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo.

Marekebisho hayo yanaipa tume uhuru wa kuhakiki matokeo, na iwapo kutakuwepo na matokeo ya kukinzana kati ya yaliyopeperushwa kwa njia ya kielektroniki na kwenye fomu zilizowasilishwa, kufanya uamuzi wa matokeo gani yatakubalika.

Mswada huo pia unazuia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi iwapo kasoro zilizoshuhudiwa si za kiwango kikubwa.

Maafisa wa tume wanaokosa kutekeleza wajibu wao kama ilivyo kwenye kanuni za tume wameongezewa adhabu pia, kutoka dola milioni moja hadi milioni mbili, pamoja na kifungo cha miaka mitano jela.

Mswada huo uliowasilishwa na mbunge wa Baringo ya Kaskazini William Cheptumo unatarajiwa sasa kuwasilishwa kwa Bunge la Seneti ambapo ukipitishwa baadaye utaidhinishwa na rais kuwa sheria.