Serikali Kenya yapiga marufuku maandamano miji mikuu

Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakiandamana kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakiandamana kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi

Serikali nchini Kenya imepiga marufuku maandamano katika maeneo ya katikati mwa miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu.

Kaimu waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i amesema pia kwamba wanaopanga maandamano wanafaa kuwajibishwa kutokana na uharibifu wa mali unaotokea wakati wa maandamano.

Hatua ya Dkt Matiang'i imetokea huku muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) wake Raila Odinga ukiendelea na maandamano ya kushinikiza mageuzi katika Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Jumatano, visa vya uporaji wa mali viliripotiwa katikati mwa jiji la Nairobi.

Mmoja wa viongozi wa Nasa James Orengo, ambaye alikuwa naibu ajenti mkuu wa Bw Odinga wakati wa uchaguzi wa mwezi Agosti ambao ulifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu, alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo kuandamana kila siku.

Muungano wa Nasa awali ulikuwa ukifanya maandamano kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza mageuzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya.

Uchaguzi ambao umepangiwa kufanyika tarehe 26 Oktoba umeingiwa na utata baada ya mgombea wa Nasa Raila Odinga kutangaza kujiondoa rasmi Jumanne.

Mapema Jumatano, Mahakama Kuu pia iliagiza mgombea wa Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot ajumuishwe kwenye uchaguzi huo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwandamanaji akiwa kwenye kidimbwi cha maji ndani ya uwanja wa Uhuru Park

Muungano wa Nasa unataka uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku 90 na wagombea wateuliwe upya.

Tume ya IEBC hata hivyo, baada ya uamuzi kuhusu Aukot, ilisema wagombea wote wanane walioshiriki uchaguzi wa tarehe 8 Agosti wataruhusiwa kuwania katika uchaguzi huo wa marudi na kwamba tarehe ya uchaguzi itasalia kuwa tarehe 26 Oktoba.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii