Wanajeshi wa Iraq waingia Kirkuk, Wakurdi watoroka

Kirkuk on Oktoba 16, 2017 Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wakitumia trekta kuharibu bango la rais wa Wakurdi Massud Barzani kusini mwa Kirkurk

Wanajeshi wa serikali ya Iraq wameingia katikati mwa mji wa Kirkuk baada ya kuteka maeneo muhimu ya mji huo unaozozaniwa kutoka kwa wapiganaji wa Kikurdi.

Maelfu ya watu waliukimbia mji huo kabla ya wanajeshi wa Iraq kufika.

Jeshi la Iraq limeingia Kirkuk wiki tatu baada ya Jimbo la Kurdistan kuandaa kura ya maoni ya uhuru.

Wanajeshi hao wanalenga kuchukua tena udhibiti wa maeneo ambayo yamekuwa yakidhibitiwa na Wakurdi tangu wapiganaji wa Islamic State walipofurushwa maeneo hayo.

Wakazi wa maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi, yakiwemo Kirkuk, waliunga mkono pakubwa kura ya maoni ya kujitenga na Iraq iliyoandaliwa 25 Septemba.

Ingawa mji wa Kirkuk unapatikana nje ya jimbo la Kurdistan nchini Iraq, wakazi wa mji huo waliruhusiwa kushiriki kura hiyo ya maoni.

Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alishutumu kura hiyo na kusema ilikuwa kinyume na katiba.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jeshi la Iraq lilitangaza kwamba limedhibiti viwanda na visima vya mafuta baada ya wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga kuondoka

Serikali ya jimbo la Kurdistan ilisisitiza kwamba ilikuwa kura halali.

Maafisa wa Marekani wamesema wanashauriana na pande zote kuzuia kuongezeka kwa uhasama.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii