Facebook yanunua app ya vijana inayovuma sana

App hiyo ya tbh app imepakuliwa zaidi ya mara 5 milioni katika kipindi cha wiki tisa Haki miliki ya picha tbh
Image caption App hiyo ya tbh app imepakuliwa zaidi ya mara 5 milioni katika kipindi cha wiki tisa

Kampuni ya Facebook imenunua programu tumishi inayowalenga vijana wa chini ya miaka 19 na kuwahimiza wawe na wema wanapohusiana.

App hiyo kwa jina tbh, ambayo ni ufupisho wa "to be honest" (kuwa mwaminifu/mkweli) imekuwepo kwa wiki tisa tu, lakini tayari imepakuliwa zaidi ya mara 5 milioni.

Waliounda programu hiyo wamesema inasalia kuwa programu ya kujitegemea lakini sasa watakwua na rasilimali zaidi kutoka kwa Facebook.

"Tulivutiwa na njia ambazo wangeweza kusaidia kutimiza ruwaza ya tbh na kuifikisha zaidi kwa watu," tbh wamesema.

Kwa mujibu wa tovuti ya TechCrunch, Facebook walinunua programu hiyo kwa "chini ya $100m", na wafanyakazi wanne waliokuwa wanaifanyia kazi tbh sasa watakuwa waajiriwa wa Facebook.

tbh wamesema ufanisi wa app hiyo unaonesha kwamba vijana wanapenda zaidi kuwa na uhusiano mwema na wa manufaa mtandaoni.

App hiyo ina kiwango fulani cha usiri.

Baada ya anayetaka kutumia app hiyo kujiandikisha, huwa anaulizwa maswali mazuri na pia kupewa fursa ya kuchagua mmoja kati ya marafiki wanne.

Wanaotumia hufahamishwa kwamba wamechaguliwa, lakini maelezo kuhusu nani aliwachagua hubaki siri.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Facebook sasa inatumiwa na watu 2 bilioni duniani

tbh inaonekana kufuata mtindo uliotumiwa na Facebook nyakati za mwanzo - ilikuwa inatumiwa na kundi ndogo la wanafunzi chuoni, kisha ikawa inapatikana kwa watu wa majimbo kadha.

Watu walipashana habari kwa maneno hadi ikaenea shule mbalimbali.

"Asilimia arobaini ya wanafunzi shuleni waliipakua siku ya kwanza. Siku iliyofuata, shule tatu zaidi na siku ya tatu shule zikafika 300," alisema mmoja wa wahusika.

Snapchat kwa sasa unaonekana kuwa mtandao unaowavutia zaidi vijana Marekani, ambao umri wa wastani kwa wanaotumia mtandao huo ni miaka 16.

Facebook walijaribu kununua Snapchat mwaka 2013 kwa $3bn. Snap, kampuni inayomiliki Snapchat, kwa sasa ina thamani ya $19bn.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii