Wakenya watoa damu kuwasaidia waathiriwa wa bomu Somalia

Baadhi ya Wakenya na wasomali waliofika katika kituo cha kutoa damu cha Eastleigh ili kuwasaidia waathiriwa wa mkasa wa bomu Somalia
Image caption Baadhi ya Wakenya na wasomali waliofika katika kituo cha kutoa damu cha Eastleigh ili kuwasaidia waathiriwa wa mkasa wa bomu Somalia

Mamia ya Wakenya pamoja na raia wa Somalia wanaoishi nchini humo walishiriki katika shughuli ya kutoa damu ili kuwasaidi wale waliojeruhiwa katika mlipuko wa bomu nchini Somalia uliowaua takriban watu 276.

Kampeni hiyo ya kutoa damu ilizinduliwa kupitia mitandao ya kijamii katika eneo la Eastleigh mjini Nairobi kufuatia bomu hilo.

Image caption Wengi walijitokeza katika kituo cha kutoa damu cha Eastleigh jijini Nairobi

Tayari takriban miili 165 isiotambulika imezikwa katika kaburi la pamoja mjini Mogadishu.

Chombo cha habari cha serikali kinasema kuwa ni watu 111 waliotambuliwa.

Baadhi ya waliojeruhiwa walisafirishwa hadi nchini Uturuki kwa matibabu zaidi kulingana na mpiga picha mmoja wa chombo cha habari cha AFP.

Hatua hiyo inajiri kufuatia ombi la serikali ya Somalia kuomba msaada wa damu .

Waziri wa habari nchini Somalia aliambia BBC kwamba idadi ya watu waliofariki huenda ikaongezeka na kwamba usaidizi zaidi ulihitajika.

Alisema kuwa zaidi ya watu 300 walijeruhiwa nchini Somalia kufuatia shambulio hilo ambalo limetajwa kuwa kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 10 huku miili kadhaa ikidaiwa kufinikwa chini ya vifusi.

Ndege mbili kutoka Marekani na Qatar zimewasili mji Mogadishu.

Image caption Raia waliokongamana katika kituo cha kutoa damu cha Eastleigh tayari wakitaka kutoa damu
Image caption Raia wakitoa damu

Serikali ya Kenya imesema kuwa itatuma tani 31 za dawa mjini Mogadishu mbali na kuwasafarisha baadhi ya waathiriwa wa mlipuko huo hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

Serikali ya Djibout nayo tayari imetuma madaktari 30 nchini Somalia wakiongozwa na waziri wa afya nchini humo ili kutoa msaada wa dharura.

Mlipuko huo wa Jumamosi ulilenga eneo lenye watu wengi na kuwaua raia wakiwemo madaktari na wanafunzi.

Image caption Hakuna kundi ambalo limekiri kuhusika lakini serikali ya Somalia inalaumu kundi la wapiganaji wa al-Shabab.

Hakuna kundi ambalo limekiri kuhusika lakini serikali ya Somalia inalaumu kundi la wapiganaji wa al-Shabab.

Shghuli ya kuchangisha damu pia inaendelea nchini Somalia ambapo maafisa wa Jeshi la AMISOM wanatoa damu.