Kampuni ya madini ya Rio Tinto yashtakiwa ulaghai Marekani kuhusu makaa Msumbiji

Coal falls from a conveyor belt Haki miliki ya picha Getty Images

Kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini ya Rio Tinto imeshtakiwa kwa tuhuma za ulaghai nchini Marekani pamoja na wakuu watendaji wake wawili wa zamani.

Kesi hiyo inahusu umiliki wa eneo la uchimbaji wa makaa ya mawe ambalo lilinunuliwa na kampuni hiyo, ambayo wamiliki wake ni kutoka Uingereza na Australia, nchini Msumbiji mwaka 2011 kwa karibu dola bilioni nne za Marekani.

Inadaiwa kwamba afisa mkuu mtendaji wa zamani wa kampuni hiyo pamoja na afisa mkuu wa zamani wa kifedha waligundua muda mfupi baada ya ununuzi kwamba eneo hilo lilikuwa na kiwango cha chini ya makaa ya mawe kuliko walivyotarajia lakini walikosa kuwaonya wawekezaji kuhusu hasara iliyotarajiwa.

Eneo hilo la uchimbaji madini baadaye liliuzwa kwa dola milioni hamsini za Marekani pekee.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Thomas Albanese ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa zamani wa Rio Tinto

Kampuni hiyo imekanusha tuhuma hizo na inasema kwamba itatetea kwa hali na mali sifa zake nzuri.

Rio Tinto pia ilitozwa faini ya £27m na serikali ya Uingereza kwa kukiuka sheria za kuweka wazi shughuli za kibiashara wakati wa ununuzi huo.

Kampuni hiyo ilikubali kulipa faini hiyo, ambayo ni ya juu zaidi kuwahi kutozwa kampuni Uingereza kuhusiana na makosa ya ufichuzi wa shughuli za kibiashara.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii