Mwigizaji wa Game of Thrones asema alidhalilishwa na Weinstein

Actress Lena Headey Haki miliki ya picha Getty Images

Mwigizaji wa mwendelezo wa filamu za Game of Thrones Lena Headey, ambaye huigiza kama Cersei Lannister, amedai mwandaaji wa filamu maarufu Hollywood Harvey Weinstein alimshalilisha kimapenzi.

Amesema Weinstein alijawa na ghadhabu alipokataa juhudi zake, kwenye maelezo ambayo ameyatoa kupitia msururu wa ujumbe kwenye Twitter.

Mwigizaji huyo wa Uingereza amejiunga na orodha ya wanawake wengine 40 ambao wamedai kudhalilishwa na mwanamume huyo.

Jumanne, Weinstein alijiuzulu kutoka kwa bodi ya wakurugenzi katika kampuni ya filamu aliyoianzisha.

Amekabiliwa na tuhuma za ubakaji, udhalilishaji wa kingono na unyanyasaji, lakini amekanusha tuhuma zote na kusema wanawake alioshiriki mapenzi nao walifanya hivyo kwa hiari.

Licha ya kufutwa wadhifa wake wa mwenyekiti wa studio za kampuni ya filamu ya Weinstein mnamo 8 Oktoba, aliendelea kushikilia nafasi kama mkurugenzi katika bodi hadi Jumanne.

Haki miliki ya picha YANN COATSALIOU
Image caption Harvey Weinstein alikuwa na ushawishi mkubwa sana Hollywood

Headey anasema alikuwa kwenye lifti na Weinstein baada yake kumwalika kwenye chumba chake (Weinstein) akatazame tamthilia.

"Lifti ilikuwa inapanda juu na alimwambia Harvey, 'Sitaki kitu kingine chochote ila kazi, kwa hivyo usidhani niko nawe hapa kwa sababu nyingine yoyote, hakuna kitakachotokea," anasema.

"Sijui nini kiliniingia wakati huo na kuniwezesha kuzungumza, lakini nilikuwa nimeamua kwamba hangenikaribia.

"Alikaa kimya baada yangu kuzungumza, akionekana mwenye ghadhabu.

"Alinitembeza hadi kwenye lifti kwa kunishika mkono kwa nguvu," anasema, na kuongeza kwamba alijihisi kama mtu "asiye na nguvu kabisa".

Baada ya hapo, anadai kwamba Weinstein alimnong'oneza na kumwambia asiambie mtu yeyote mwingine kuhusu yaliyotokea.

Ameandika: "Niliingia kwenye gari langu na kulia."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii