Idadi ya waliouawa na bomu Somalia yafikia 358

Mlipuko wa bomu Somalia uliowauawa zaidi ya watu 350
Image caption Mlipuko wa bomu Somalia uliowauawa zaidi ya watu 350

Serikali ya Somalia inasema kuwa idadi ya watu waliokufa katika shambulio kubwa la bomu la ndani ya Lori katika mji mkuu Mogadishu Jumamosi iliyopita imeongezeka na kufikia hadi watu 358 .

Lori lililipuka katika barabara ya makutano yenye shughuli nyingi na kuharibu hoteli, ofisi za serikali na migahawa .

Hata hivyo haijabainika ikiwa eneo hilo la makutano ndilo lililolengwa au dereva wa Lori alilipua vilipuzi kwa sababu tayari watu walikuwa wameanza kushuku lori lake .

Maafisa wamelilaumu kundi la wanamgambo wa al-Shabaab kwa shambulio hilo , lakini kundi hilo bado halijasema kuwa lilihusika na mlipuko huo

Mlipuko huo ulikuwa umewawacha takriban watu 228 wamejeruhiwa ambapo 122 kati yao walikuwa wamesafarishwa nchini Uturuki, Sudan na Kenya kwa matibabu.

Somalia imekuwa ikitoa wito wa ufadhili wa damu ili kuwatibu majeruhi.

Image caption Mwathiriwa wa shambulio la bomu Somalia akinusuriwa

Zaidi ya waathiriwa 150 walichomwa hadi kutoweza kutambulika na walizikwa na serikali siku ya jumatatu.

Raia wa Somalia mjini Mogadishu wamefanya maandamano dhidi ya al-Shabab kufuatia shambulio hilo, huku wengi wakivaa vilemba vyekundu katika vichwa vyao ili kuonyesha umoja wao na waathiriwa.

Wanajeshi 22,000 wa Umoja wa Afrika wako nchini humo ili kujaribu kuisaidia serikali kuyateka maeneo yaliotekwa na al-Shabab ambao wapiganaji wake hutekeleza mashambulio mashambani mwa kusini mwa Somalia.

Mada zinazohusiana