Uchaguzi 2017: Mabalozi wa Magharibi wawaonya wanasiasa Kenya

Karatasi za kura Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tume imeendelea na maandalizi ya uchaguzi huo wa Alhamisi

Mabalozi kutoka nchi za Magharibi nchini Kenya wamewataka wanasiasa nchini humo kuachana na "tabia hatari" huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda kabla ya uchaguzi wa marudio kufanyika Alhamisi.

Katika taarifa yao wanadiplomasia hao wamesisitiza kuwa uchaguzi wa urais unafaa kufanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Mabalozi hao, wakiongozwa na balozi wa Marekani Robert Godec aidha wamewataka wanasiasa kutoa wito kwa wafuasi wao kutowashambulia maafisa wa tume ya uchaguzi.

Wamemtaka rais Uhuru Kenyatta kutotia saini marekebisho ya sheria za uchaguzi ambayo yalipitishwa hivi majuzi na Bunge linalodhibitiwa na chama chake cha Jubilee.

"Suluhu ya changamoto za sasa Kenya lazima zipatikane kwa kufuata katiba, sio nje ya katiba. Ni katiba pekee inayohakikisha haki kwa wote, na sio kwa wenye mali na mamlaka pekee.

"Uchaguzi huu ni sharti ufanyike kwa kufuata Katiba na sheria, kama zilivyofasiriwa na mahakama.

"Majaribio la kubadili sheria dakika za mwisho hayatasaidia, na kwa mara nyingine tunamhimiza Rais Kenya kutotia saini marekebisho ya sheria za uchaguzi."

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Rais Kenyatta alikutana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mapema laoe

Katika mkutano wake na mkuu wa tume ya uchaguzi IEBC hivi leo, Rais Kenyatta ameendelea kuisisitiza kuwa tume hiyo iandae uchaguzi uliopangwa kufanyika 26 Oktoba.

Tayari kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga alishatangaza kutoshiriki uchaguzi huo na badala yake amewataka wafuasi wa muungano wake wa National Super Alliance (Nasa) kuandamana siku hiyo.

Bw Godec amesema walisikitishwa sana na hatua ya Bw Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka kujiondoa kutoka kwenye uchaguzi na kwamba wamekuwa wakijaribu kuwashawishi kukubali kushiriki uchaguzi huo na "tunaendelea kutumai kwamba watafanya hivyo ukizingatia hatua zilizopigwa na IEBC na kujitolea kwetu kwa pamoja kufanikisha uchaguzi huru wa kidemokrasia."

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Odinga amesisitiza kuwa hatashiriki uchaguzi huo

Mabalozi hao, wakiwemo Nic Hailey wa Uingereza, Jutta Frasch wa Ujerumani na Stefano A. Dejak wa Umoja wa Ulaya pia wametoa wito kwa polisi kutotumia nguvu kupita kiasi wakikabili waandamanaji.

Muungano wa upinzani Nasa umekuwa ukiandaa maandamano ya mara kwa mara kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi.

Baada ya kuyaahirisha kwa muda, wakuu wa muungano huo wametangaza kwamba maandamano yataanza tena Jumanne katika miji mikubwa nchini humo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii