Aliyemgusa mwanamume kwenye kiuno Dubai asamehewa

Jamie Harron Haki miliki ya picha Detained in Dubai/Getty
Image caption Jamie Harron

Mwanamume mmoja raia wa Scotland ambaye alishtakiwa kwa upotovu wa maadili mjini Dubai amesamehewa baada ya mfalme wa mji huo kuingilia kati.

Jamie Harron, 27, kutoka Stirling alikuwa amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela kwa kumguza kiunoni mwanamume mwingine wakiwa kwenye baa.

Kundi linalomuakilisha Bw. Harron huko Dubai linasema kuwa alisamehewa na Sheikh Mohammed bin Rashid al-Maktoum.

Lilisema kuwa Bw. Harron alirejeshewa paspoti yake na yuko huru kuondoka Dubai.

Bw. Harron pia alikuwa amelaumiwa kwa kunywa pombe na kufanya ishara mbaya dhidi ya mfanyabiashara ambaye alitoa malalamiko.

Bw. Harron alikamatwa mwezi Julai na kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu katika eneo la umma.

Anasema kuwa alikuwa anajaribu kuzuia kumwaga kinywaji chake wakati alimgusa kimakosa mwanamume huyo.

Mwanamume ambaye alikuwa amelalamika kuhusu tabia ya Bw. Harron, aliondoa kesi lakini waendesha mashtaka wakaendelea na kesi hiyo.

Bw. Harron ambaye alikuwa anafanya kazi nchini Afghanistan, alikuwa amesima Dubai kwa muda wa siku mbili wakati wa kisa hicho.

Alisema alipoteza kazi yake na kutumia zaidi ya dola 30,000 kwa kesi hiyo.