Serikali ya Tanzania yalifungia gazeti la Daima kwa siku 90

Gazeti la Daima lafungiwa kwa siku 90
Image caption Gazeti la Daima lafungiwa kwa siku 90

Serikali ya Tanzania kupitia idara ya habari maelezo imelifungia gazeti la Tanzania Daima ambalo ni gazeti la kila siku, kwa muda wa siku 90 .

Tamko hilo pia limepiga marufuku toleo la mitandaoni la gazeti hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji mkuu wa serikali Tanzania Dr, Hassan Abbas, amesema gazeti hilo limefungiwa kutokana na ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya habari ikiwemo kuchapisha habari za uongo na za kichochezi ambazo zinaweza kuzusha hofu miongoni mwa jamii.

Miongoni mwa habari zilizosababisha kufungwa kwa gazeti la Tanzania Daima , ni ile iliyokuwa na makosa ya kihariri kwenye toleo nambari 4706 la Oktoba 22, 2017 ambalo liliandika kuwa 'ASILIMIA 67 YA WATANZANIA WANATUMIA ARVS' dawa za kufubaza makali ya ugonjwa wa ukimwi.

Habari nyingine katika toleo hilo ilieleza kuwa "MAKINIKIA PASUA KICHWA".

Idara hiyo imedai kuwa gazeti hilo limetoa habari yenye uongo wenye nia ya kuleta dharau dhidi ya hatua ya serikali na makubaliano yaliyofikiwa baina yake na kampuni ya Barrick Gold Corporation.

Tanzania Daima, linakuwa gazeti la nne kufungiwa na serikali ya Tanzania ndani ya miezi minne ikiwemo gazeti la Raia Mwema na Mwana Halisi lililofungiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa ni uchapishaji wa habari za uongo na kichochezi ambazo zingeweza kuhatarisha usalama wa taifa hilo.

Image caption Gazeti la Daima nchini Tanzania

katika siku za hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikimulikwa kwa karibu nchini Tanzania.

Ikumbukwe kwamba mapema mwaka huu Raisi Magufuli alivionya vyombo vya habari nchini humo 'visifikiri kwamba viko huru kwa kiwango hicho.' kauli ambayo inatoa angalizo la umakini katika kazi za kila siku za vyombo hivyo kwa muujibu wa sheria ya mitandao na sheria za Tanzaia.

Mada zinazohusiana