Mshukiwa anayedaiwa kumnajisi msichana wa miaka minne asamehewa Ghana

#Justice4Her
Image caption Watu wamekuwa wakitumia kitambulisha mada #JusticeForHer kushinikiza hatua zichukuliwe

Inspekta Mkuu wa polisi nchini Ghana amewaamuru polisi nchini humo kufanya uchunguzi kuhusu kisa cha kunajisiwa kwa mtoto wa miaka minne ambacho kimeshutumiwa vikali nchini humo.

Wazazi wa mtoto huo walisema chifu wa eneo lao aliwaambia hawezi kuchukua hatua yoyote kwa kuwa miungu wa jamii hiyo walisema mshukiwa hana makosa.

Wengi wanasema kisa hicho kinadhihirisha utamaduni wa kuwalinda watuhumiwa wa ubakaji na unajisi.

Polisi wa eneo hilo sasa wanachunguzwa pia kwa tuhuma za kuzembea wakati wa kufanya uchunguzi wa kisa hicho.

Mkuu wa polisi wa Ghana David Asante-Apeatuhas amemwita kamanda wa polisi wa Jimbo la Kati ajibu maswali kuhusiana na jinsi polisi walivyoshughulikia kisa hicho.

Mshukiwa ambaye ana miaka 18 bado hajakamatwa tangu habari za kisa hicho zilipochipuka karibu wiki mbili zilizopita, mwandishi wa BBC Thomas Naadi aliyepo Accra anasema.

Kisa hicho kimeibua malalamiko huku watu wakitumia kitambulisha mada #JusticeForHer (Haki kwake) kwenye mitandao ya kijamii kushinikiza hatua zichukuliwe.

Kuna pia shutuma kuhusu mtazamo wa kiongozi huyo wa kitamaduni kuhusu unajisi huo.

Watu wamechanga $4,000 (£3,050) za kutumiwa kumfanyia upasuaji msichana huyo ambaye ameruhusiwa kuondoka hospitalini.

Angela Dwamena-Aboagye, wakili na mtetezi wa kuwezeshwa kwa wanawake, ameambia BBC kwamba hatua hiyo ya polisi inasikitisha.

Mada zinazohusiana