Watu watatu wauawa maandamano dhidi ya Kabila DR Congo

Kabila Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tume ya uchaguzi DR Congo imesema haiwezi kuandaa uchaguzi mwaka huu

Watu watatu akiwemo afisa wa polisi wameuawa katika maandamano ya kupinga serikali katika mji wa Goma mashariki mwa DRC.

Mashirika ya kiraia yameitisha mgomo wa kitaifa na yanashinikiza rais Joseph Kabila ajiuzulu kabla ya Novemba 30.

Waandamanaji walifunga barabara mjini humo wakitumia mawe.

Muhula wake ulimalizika Desemba mwaka jana lakini tume ya uchaguzi nchini humo inasema uchaguzi hauwezi kufanyika mpaka mwaka 2019.

Katika taarifa tume ilisema kuwa inahitaji takriban siku 504 kuweza kuandaa uchaguzi huo mara usajili wa wapiga kura utakapokamilika

Tangazo la tume hiyo linaenda kinyume na maafikiano yaliyopatikana baada ya maandamano mengine mwaka jana kwmaba uchaguzi nchini humo unafaa kuandaliwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley alipozuru nchi hiyo wiki iliyopita alisema serikali ya Rais Kabila inafaa kuandaa uchaguzi iwapo inatarajia kuendelea kupata uungwaji mkono wa Marekani.

Mada zinazohusiana