Donald Trump ataka mshukiwa wa mauaji New York kuhukumiwa kifo

Muuaji wa New York Sayfullo Saipov
Maelezo ya picha,

Muuaji wa New York Sayfullo Saipov

Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza wito wa mshukiwa wa shambulio la mjini New York kupewa hukumu ya kifo.

Lakini Trump alipuuzilia mbali wito wake wa hapo awali wa kutaka mshukiwa huyo Sayfullo Saipov kupelekwa Guantanamo Bay akisema mpango huo unachukua muda mrefu.

Mshukiwa huyo aliwaambia maafisa wa polisi kwamba, alijihisi vyema baada ya shambulio hilo la halloween na alitaka kuwaua watu wengi zaidi.

Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 29 aliendesha gari alilokuwa amekodisha katika eneo la barabara ya waendesha baiskeli na kuwaua watu wanane.

Waathiriwa walikuwa raia 5 wa Argentina ambao walikuwa wamesafiri hadi mjini New York kusherehekea miaka 30 tangu kuhitimu kwao katika shule yao ya upili pamoja na mama mmoja raia wa Ubelgiji na raia wawili wa Marekani.

Bwana Saipov ambaye ni muhamiaji wa Uzbek alipigwa risasi na maafisa wa polisi katika eneo la tukio , kulingana na maafisa.

Wachunguzi wanasema kuwa anadai kushinikizwa na kundi la wapiganaji wa Islamic State.