Odinga awataka wafuasi kususia bidhaa za kampuni tatu Kenya

Odinga

Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) umetoa wito kwa wafuasi wake kususia bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni tatu ambazo unadai zimekuwa zikimpendelea Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Kenyatta alitangazwa Jumatatu kuwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika 26 Oktoba, ambao kiongozi wa Nasa Raila Odinga alisusia akisema haungekuwa huru na wa haki.

Bw Odinga alitangaza kabla ya uchaguzi huo kwamba muungano huo utabadilika na kuwa Kundi la Pingamizi dhidi ya Serikali na baadhi ya hatua ambazo ulisema utachukua ni kususia bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni ambazo alidai zinamfaa Bw Kenyatta.

Kampuni ambazo Nasa wamesema wafuasi wao wanafaa kususia ni:

•Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, ambayo ndiyo tajiri zaidi miongoni mwa kampuni za Kenya

•Kampuni ya maziwa ya Brookside, inayomilikiwa na familia ya Kenyatta

•Kampuni ya kutengeneza mafuta ya kupikia na sabuni ya Bidco

Safaricom leo ilitangaza Safaricom kukua kwa faida yake baada ya kutozwa ushuru kwa kipindi cha nusu mwaka kilichomalizika tarehe 30 Septemba kwa asilimia 9.5 hadi Sh26.2 bilioni.

Kampuni hizo kufikia sasa hazijazungumzia hatua hiyo ya upinzani ya kuwataka Wakenya kususia bidhaa na huduma zao.

Bw Odinga alisusia kushiriki uchaguzi huo wa mwezi uliopita akishinikiza mageuzi yafanywe kwanza katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Uchaguzi huo ulitokana na hatua ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ikisema ulikuwa na kasoro nyingi.

Mahakama hiyo ilikuwa inatoa uamuzi katika kesi iliyokuwa imewasilishwa na Bw Odinga kupinga matokeo hayo.

Bw Kenyatta alishinda uchaguzi huo wa marudio kwa kura 7.5 milioni ambazo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa.

Idadi ya waliojitokeza ilikuwa ni asilimia 38.84 ya waliokuwa wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo.

Matokeo kamili ya wagombea wote kama yalivyotangazwa na IEBC

Uchaguzi ulitatizika sana katika maeneo yenye wafuasi wengi wa upinzani. Katika majimbo manne magharibi mwa Kenya ambayo ni ngome ya Bw Odinga, uchaguzi uliahirishwa kwa siku kadha na baadaye haukufanyika.

Nasa wameituhumu Safaricom - ambayo ilikuwa imepewa kazi ya kupeperusha matokeo na tume ya uchaguzi kutoka vituo vya kupigia kura hadi kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo - kwa kushiriki katika njama ya kuchakachua matokeo.

Safaricom imekanusha tuhuma hizo.

Zaidi ya 90% ya simu zinazopigwa nchini Kenya hupigwa kupitia mtandao wa Safaricom, ambayo ni maarufu sana kutokana na huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu, M-Pesa.