Mshirika wa Trump Wilbur Ross ahusishwa na kampuni za Urusi zilizowekewa vikwazo

Wilbur Ross has played a key part in Donald Trump's business and political careers

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wilbur Ross amekuwa mtu muhimu katika biashara za Donald Trump na katika siasa zake

Mwanachama wa ngazi ya juu katika uongozi wa Donald Trump anafanya biashara na warusi walio na uhusiano na rais Vladimir Putin, ambao wamewekewa vikwazo na Marekani, kwa mujibu wa ufichuzi wa nyaraka unaojulikana kama Paradise Papers.

Waziri wa biashara Wilbur Ross ana hisa katika kampuni ya Navigator Holdings ambayo hupata mamilioni ya dola kila mwaka kwa kusafirisha mafuta na gesi kutoka kwa kampuni ya mafuta ya Urusi, Sibur.

Wenye hisa wakuu wa kampuni ya Sibur wamewekewa vikwazo na Marekani.

Mtu mwingine mwenye hisa ni mkwe wa rais Putin, Kirill Shamalov.

Maelezo ya picha,

Uhusiano wa Wibur na Urusi

Ana asilimia 3.2 katika kampuni hiyo. Gennady Timcheno ambaye binafsi amewekewa vikwazo na Marekani ana takriban kampuni 12 zenye uhusiano naye, na Leonid Mokhelson ambaye kampuni yake kuu, Novatek pia imewekewa vikwazo, ni washika dau wakuu.

Msemaji wa wizara ya biasshara alisema kuwa Bw. Ross aliwahi kukutana na washika hau hao watatu wa Urusi.

Marekani ilitangaza vikwazo kadhaa baada ya Urusi kulimega eneo la Crimea mwaka 2014. Vingine vilitangazwa mwaka uliopita kwa madai ya kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani.

Ufichuzi huo tena utaibua maswali kuhusu uhusiano wa Urusi na timu ya Trump.

Uongozi wake umekumbwa na madai kuwa Urusi ilihusika katika kushawishi matokeo ya uchaguzi wa Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Donald Trump akiwa katika casino ya Taj Mahal casino mwaka 1990

Wilbur Ross na Donald Trump wamejuana kwa zaidi ya robo karne. Bw Ross alishiriki pakubwa katika makubaliano kati ya kampuni ya kamari cha Trump ya Taj Mahal na wakopeshaji wake miaka ya tisini.

Kampuni ya WL Ross & Co ambayo ilianzishwa na Wilbur Ros, mara ya kwanza iliwekeza katika kampuni ya Navigator Holdings mwaka 2011.

Uchunguzi umefichua taarifa kuhusu vile Bw. Ross ni mshika dau katika kampuni ya Navigator Holdings kupitia kampuni kadhaa na visiwa vya Cayman.

Baadhi ya kampuni hizo za Cayman zilifichuliwa na Bw. Ross wakati aliteuliwa waziri wa biashara.