Magufuli: Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo wa taifa jirani

Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya taifa jirani
Maelezo ya picha,

Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya taifa jirani

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwakamata mifugo watakaoingia nchini humo kutoka taifa jirani.

Akizungumza katika mkoa wa Kagera ambako ameanza ziara yake ya kikazi Magufuli amesema kwamba Tanzani sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani na kwamba ataichukulia mifugo hatua kali za kisheria mifugo yoyote.

Vilevile ameitaka nchi Jirani kuchukua hatua kama hiyo iwapo mifugo ya Tanzania itaingia nchini humo kinyume na sheria.

Maelezo ya sauti,

Tanzania kuwapiga mnada zaidi ya ng'ombe 1000 kutoka Kenya

"Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani, ndio maana tumeamua kukamata mifugo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kisheria, na hata huko kwenye nchi jirani wakishika mifugo ya kutoka Tanzania wachukue hatua za kisheria za nchi hizo" alisisitiza rais Magufuli.

Matamshi hayo ya Magufuli yanajiri wakati ambapo kumekuwa na mgogoro wa mpakani mwa Kenya na Tanzania kuhusu mifugo katika siku za hivi karibuni.

Maelezo ya sauti,

Wafugaji wa Kenya wapata hasara kwa kuingiza ngombe zao Tanzania

Wiki tatu zilizopita serikali ya Tanzania ilizikamata zaidi ya ng'ombe 1000 kutoka Kenya na baadaye mahakama moja nchini humo ikaamuru mifugo hao kupigwa mnada na fedha hizo kutumiwa na serikali iwapo wamiliki wa ng'ombe hizo watashindwa kulipa faini ya shilingi milioni 500 za Tanzania.

Maelezo ya picha,

Mifugo ya jamii ya Maasai nchini Kenya

Na wiki moja iliopita takriban ng'ombe 4000 kutoka Tanzania zilidaiwa kupatikana katika jamii moja ya Maasai mjini kajiado.

Hivi majuzi hatua ya taifa la Tanzania kuwachoma kuku 6,400 kutoka Kenya wenye thamani ya shilini milioni 12 za Tanzania kwa madai kwamba wangesambaza ugonjwa wa homa ya ndege ilizua hizo tofauti kutoka kwa watetezi wa wanyama .

Afisa mkuu wa maswala ya mifugo nchini Tanzania Obedi Nyasembwa alisema kuwa kuku hao waliingizwa nchini humo kinyume na sheria na kwamba uwpo wao nchini humo ulikuwa hatari kwa ndege wengine.

Maelezo ya sauti,

Vifaranga wa kuku 6,400 wenye thamani ya zaidi ya dola 5,000 wamechomwa moto Tanzania

Kuku hao wa siku moja walikamatwa katika eneo la Namanga huku mfanyibishara wa Tanzania akikamatwa.

Baadaye mamlaka ya Tanzania iliwamwagia mafuta na kuwachoma kulingana na gazeti la mwananchi.

Aidha rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Kagera kuhakikisha kuwa mifugo yao inawekwa alama kwa mujibu wa sheria, ili kurahisisha utambuzi wa mifugo inayoingizwa nchini kutoka nchi jirani na pia kudhibiti ruzuku inayotolewa na Serikali kwa dawa za mifugo za hapa nchini.

Maelezo ya picha,

Kuku hao wa siku moja walikamatwa katika eneo la Namanga huku mfanyibishara wa Tanzania akikamatwa.

Hata hivyo amewataka wananchi wa Kagera kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ikiwemo hifadhi ya Burigi na ameagiza viongozi wa Wilaya ya Muleba kufuatilia madai ya wananchi juu ya kuuzwa kwa ardhi ya kijiji hatu iliosababisha wananchi kukosa maeneo ya kulima na kulisha mifugo yao.

"Na kuna watu waliouziwa ranchi na Serikali, watu hao hawajaziendeleza ranchi hizo na badala yake wanawakodisha wananchi, wafuatilieni na mkiona hawajaziendeleza nyang'anyeni muwape wananchi wazitumie kwa ufugaji, lakini pia hakikisheni wananchi hawavamii maeneo ya hifadhi yaliyotengwa" aliongeza Magufuli