Nyaraka za Paradiso: Nani anadhibiti klabu ya Everton?

Wayne Rooney and Alexis Sanchez

Chanzo cha picha, PA/ Getty Images

Maelezo ya picha,

Sheria za Ligi ya Premia huwa makini sana kuhusu umiliki wa klabu

Maswali yameibuka kutokana na na nyaraka za ufichuzi ambazo zimepewa jina Nyaraka za Paradiso kuhusu nani hasa anayemiliki klabu ya Everton FC na iwapo sheria za Ligi ya Premia zilivunjwa.

Farhad Moshiri aliuza hisa anazomiliki katika klabu ya Arsenal mwaka 2016 na kununua karibu 50% ya hisa za Everton.

Lakini nyaraka hizo zilizovunja zinadokeza kwamba hisa asili alizokuwa anamiliki Arsenal alikuwa amezipata kama "zawadi" kutoka kwa tajiri Alisher Usmanov, anayemiliki 30.4% ya hisa za Arsenal, jambo linaloibua maswali kuhusu iwapo pesa hizo zilifika Everton.

Bw Moshiri amekanusha kwamba alipokea pesa hizo kama zawadi.

Mawakili wake waliomuwakilisha katika mkataba huo wake na Everton wamesema tuhuma zozote kwamba sheria za Ligi ya Premia zilivunjwa ni za uongo.

Wanasema Bw Moshiri kivyake ni tajiri na alifadhili uwekezaji wake katika kandanda kivyake.

Wanasheria wanaomuwakilisha Usmanov wamesema kuna makosa kwenye tuhuma hizo na kwamba uchunguzi huo ulikuwa ni kuingilia usiri wa mteja wao.

Sheria za Ligi ya Premia zinasema mtu binafsi anayemiliki zaidi ya 10% ya hisa katika klabu moja hawezi kuwa na hisa hata moja katika klabu nyingine inayocheza ligi hiyo, kuzuia mgongano wa maslahi, kwenye uchezaji wa mechi na kuhama kwa wachezaji.

Kirasmi, Bw Usmanov na Bw Moshiri, mhasibu wa zamani wa tajiri huyo, alinunua 14.58% ya hisa Arsenal mwaka 2007 kupitia kampuni iliyosajiliwa katika visiwa vya nje ya nchi inayoitwa Red and White Holdings.

Lakini nyaraka zinaonyesha kwamba fedha zote zilizotumiwa wakati wa ununuzi wa hisa hizo za Arsenal zilitoka kwa kampuni kwa jina Epion Holdings, ambayo inamilikiwa yote na Bw Usmanov, ambaye anadaiwa kuwa na mali ya thamani ya $15.8bn (£12bn) kwa sasa.

Stakabadhi moja inasema: "Mgawo wa faida kutoka kwa Gallagher Holdings kwenda kwa Alisher Usmanov ambaye atatoa pesa hizo kama zawadi kwa Moshiri ambaye naye atawekeza katika kampuni hiyo. Fedha za Red and White zimetoka kwa Epion Holdings Limited".

Gallagher Holdings pia humilikiwa na Usmanov.

NYARAKA HALISI

Mawakili waliomwakilisha Bw Moshiri mwanzoni walikanusha kwamba pesa zilitoka kwa Epion.

Lakini baadaye walikiri kwamba pesa asili zilitoka kwa Epion, lakini walisema Bw Moshiri hatimaye alimlipa Bw Usmanov pesa zake.

Red and White Holdings wameendelea kuongeza hisa wanazomiliki Arsenal, na kufikia 30.4%.

Februari 2016, Bw Moshiri aliuza nusu ya hisa zake Arsenal kwa tajiri huyo wa Urusi.

Stakabadhi katika Nyaraka za Paradiso kutoka kwa Appleby, kampuni iliyosimamia kukamilishwa kwa mkataba huo, inathibitisha kwamba uuzaji huo ulifanyika ili kupata pesa za kununua 49.9% ya hisa Everton. Bei yake iliripotiwa kuwa £87.5m.

Kampuni moja ya habari ya Urusi ambayo ina uhusiano wa karibu na Bw Usmanov awali ilikuwa imeripoti kuhusu mkataba huo wa Everton kwamba "Mfanyabiashara wa Urusi Alisher Usmanov amekuwa mmiliki mpya wa Everton".

Taarifa hiyo iliondolewa upesi lakini tayari maswali yalikuwa yameibuka.

Shaka ziliibuka zaidi Januari ilipotangazwa kwamba uwanja wa mafunzo wa Everton, Finch Farm, sasa ulikuwa unadhaminiwa na kampuni ya Bw Usmanov, USM Holdings.

Uwanja huo baadaye ulibadilishwa jina na kuwa USM Finch Farm.

BBC Panorama walipowasiliana an Bw Moshiri na kumwuliza iwapo Bw Usmanov ndiye aliyekuwa anadhibiti Everton, aliuliza: "Mna wazimu? Mmemuona daktari wa magonjwa ya kiakili?"

Alisema: "Iwapo ni mkopo, unadaiwa pesa naye. Iwapo ni zawadi, basi ni zako pesa hizo. Si moja kati ya hizo kwa sababu nilimlipa."

Bw Moshiri baadaye alsiema nyaraka zote zilizozungumzia pesa hizo kama zawadi zilikuwa na makosa.

Wawakilishi wa Bw Moshiri kisheria katika Ligi ya Premia walikuwa wamefanya uchunguzi, ikiwa ni pamoja na ufadhili, na walijiridhisha kwamba walitii sheria kuhusu Umiliki na Ukurugenzi wa klabu.

Pia walisema Bw Moshiri, ambaye anadaiwa na jarida la Forbes kuwa na utajiri wa $2.4bn, alikuwa baadaye ametoa fedha nyingi zaidi kwa Everton.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka England Greg Dyke aliambia Panorama kwamba suala la zawadi "si la kawaida", na akaongeza, "Iwapo nyaraka hizi zinasema mnachosema kwamba zinasema, basi ninahisi kwamba Ligi ya Premia itataka kufanya uchunguzi wake binafsi."

Waziri wa utamaduni wa upinzani Tom Watson amesema atawaandikia barua Ligi ya Premia kuwaomba wafanye uchunguzi.

Matokeo ya uchunguzi wowote yatategemea yale ambayo wanaume hao wawili walifanya na yale ambayo klabu hizo mbili zilifahamu.

Walipoulizwa kuhusu hilo, Ligi ya Premia walisema hawatafichua "taarifa za kisiri kuhusu klabu au watu binafsi".

Mkataba huo wa Everton ulifanikishwa na kampuni ya Bridgewaters Limited iliyosajiliwa Isle of Man.

Stakabadhi nyingine katika Nyaraka za Paradiso zinazokeza kwamba kampuni ya Bridgewaters ilitwaliwa kimya kimya na Bw Usmanov mwaka 2011.

Tuhuma hizo zinakanushwa na Bridgewaters na Bw Usmanov.

Blue Heaven Holdings, kampuni inayomiliki Everton, ina afisi ambayo imesajiliwa Bridgewaters na wakurugenzi wake wawili ni mwajiriwa wa Bridgewaters na mwajiriwa wa kampuni ya Bw Usmanov, USM Holdings.

Alisher Usmanov ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Alizaliwa Uzbekistan mwaka 1953, na ana uraia wa Urusi
  • Amepewa jina la utani "mwanamume mgumu wa urusi", na alipata utajiri wake wa kwanza akifanya biashara ya plastiki, madini na chuma
  • Amebadilisha uwekezaji wake miaka ya karibuni na kuwekeza zaidi katika mitandao ya kijamii, simu za rununu na uchapishaji
  • Anamiliki 30.4% ya hisa Arsenal FC. Hutoa pesa nyingi sana za hisani
  • Alipatikana na makosa na kufungwa katika Muungano wa Usovieti mwaka 1980 kutokana na mkosa ya ulaghai na wizi wa mali ya umma lakini Mahakama ya Juu Uzbekistan ilibatilisha hukumu hiyo mwaka 2000, na kusema ushahidi ulikuwa wa kughushi
  • Ametetea sifa zake sana. Alimshtaki kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny kuhusu tuhuma za rushwa na alitoa simu za rununu bure kwa michoro ya utani bora zaidi iliyomfanyia utani
  • Mwaka 1992 alimuoa mkufunzi wa sarakasi Irina Viner, anayedaiwa kuwa mwandani wa karibu wa Vladimir Putin

Mawakili wa Bw Usmanov wamesema kulikuwa na "makosa ya ukweli na ufasiri" katika tuhuma zilizotolewa, lakini hawakutoa maelezo zaidi.

Walisema: "Mteja wetu hana wajibu kwa vyovyote vile kuwasaidia katika uchunguzi wenu. Sisi yeye bali nyinyi ndio mnafaa kufanya utafiti kama wanahabari ambao kimsingi unaonekana kuwa wa kupotosha."

Mei, Usmanov alishindwa katika juhudi zake za kutaka kutumia £1bn kununua hisa za mwenyehisa mkuu wa Arsenal Stan Kroenke, hatua ambayo ingemfanya kumiliki 97% ya hisa za Arsenal.

Bw Usmanov anaaminika kusikitishwa sana na kushindwa kwake kuwa na usemi katika maamuzi Arsenal kwani hana mwakilishi kwenye bodi.

Klabu zote mbili zimekuwa na matatizo uwanjani.

Wengi wa mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakiulizwa iwapo Arsene Wenger anafaa kuruhusiwa kuendelea kufanya kazi ikizingatiwa kwamba amekaa kwa muda bila kushinda ligi, Everton nao walimfuta Ronald Koeman baada ya mwanzo mbaya msimu huu.

Klabu hizo mbili zilikutana Goodison Park mnamo 22 Oktoba, ambapo Arsenal walishinda 5-2.

Nyaraka hizi ni mkusanyiko mkubwa wa nyaraka zilizofichuliwa nyingi ambazo ni kutoka kwa kampuni ya uanasheria ya Appleby, pamoja na sajili za kampuni katika maeneo 19, ambazo zinafichua shughuli za kibiashara za wanasiasa, wasanii na wachezaji mashuhuri, kampuni kubwa na viongozi duniani.

Nyaraka hizo takriban 13.4 milioni zilikabidhiwa gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung na kisha zinakabidhiwa shirika la wanahabari wapekuzi wa kimataifa International Consortium of Investigative Journalists (ICIJ). Panorama imeongoza utafiti kuhusu nyaraka hizo kwa niaba ya BBC kama sehemu ya uchunguzi mkubwa wa kimataifa ulioshirikisha mashirika mengine karibu 100 ya habari, yakiwemo Guardian, katika nchi 67. The BBC haifahamu chanzo cha nyaraka hizi.