Wezi wa nywele wanavyowahangaisha watu Kashmir

Mwanamke wa kiislamu wa Kashmiri anaonyesha nywele zake zilizokatwa alipokuwa amepoteza fahamu

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Tasleema Rouf, mwenye umri wa miaka 35, alikuwa juu ya nyumba yake ya ghorofa, katika eneo la Srinagar, jimbo la Kashmir, upande unaotawaliwa na India, alipoona kivuli cha mwanamume.

Kabla hajafanya lolote, alishambuliwa. Alijaribu kupiga mayowe na kuitisha usaidizi lakini mshambulizi wake alimnyonga. Alizirai.

Hivyo ndivyo mume wake alimpata - akiwa amelala sakafuni na nywele zake zikiwa zimekatwa.

Zaidi ya visa 40 vya watu kushambuliwa na kukatwa nywele vimeripotiwa katika majimbo ya Jammu na Kashmir kutoka tarehe 6 Septemba, jambo ambalo limesababisha hali ya taharuki na wasiwasi. Ni tukio ambalo lilisababisha hata vyuo na shule kadhaa kufungwa kwa muda.

Hii sio mara ya kwanza kwa visa vya watu kukatwa nywele kugonga vichwa vya habari India. Zaidi ya wanawake 50 kutoka majimbo ya Haryana and Rajasthan waliripoti mwezi Agosti kuwa nywele zao zinakatwa wakiwa wamepoteza fahamu.

Lakini kwa sababu ya uhusiano mbaya kati ya kashmir na serikali ya india, mashambulizi haya yamesababisha vurugu na vidole vya lawama kunyooshewa maafisa wa usalama wa India na wanaotaka kujitenga.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Maelezo ya picha,

Tasleema Rouf anaonekana akilia baada ya kushambuliwa na kukatwa nywele

Haijulikani ni nani anatekeleza mashambulizi haya. Waathiriwa wanasema waligongwa na wakapoteza fahamu na walipopata fahamu walikuwa wamekatwa nywele. Wengine wanasema waliowashambulia walikuwa wamejifunika uso. Hakuna hata mmoja kati yao aliyemwona mshambulizi wake.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Mwanamke huyu ambaye hakutaka kutambulika, alikubali kupigwa picha akiwa amelala kando ya nywele zake zilizokatwa.

Anasema alishambuliwa nje ya nyumba yake asubuhi mapema. Mkufu wake wa dhahabu ulichukuliwa lakini aliyemshambulia hakubeba nywele aliyokata - kama tu kwenye matukio yale mengine, nywele iliachwa nyuma.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Visa hivi vimezua wasiwasi katika jimbo hilo na kusababisha maandamo. Chama tawala cha India, Bharatiya Janata Party (BJP), ambalo linagawanya mamlaka na chama cha People's Democratic Party (PDP) katika majimbo ya Jammu na Kashmir, kimedai kuwa matukio haya yanatumiwa na wanaotaka kujitenga na wanaopinga taifa kama njia ya kuvuruga amani". Kimetaka mahakama kuchunguza.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Mwanaharakati Ahsan Antoo alikashifu mashambulizi hayo yanayoonekana kama udhalilishaji wa wanawake wa Kashmiri. Chama pinzani, National Conference party kimeishutumu serikali kwa kukosa kulinda "heshima" ya "mama, dada na watoto wao wa kike." Hata kikundi cha wanamgambo cha Hizbul Mujahideen kimedai kuwa hii ni njama ya serikali ya India ya kupambana na wanamgambo kwani wanakijiji walio na hofu sasa watatoa ripoti kuhusu wanamgambo wanaopita vijijini mwao.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Waandamanaji wamekuwa wakikabiliana na polisi kila mara. Sasa idara ya polisi imezindua kitengo spesheli cha kuwakamata washambulizi. Vilevile wametangaza tuzo ya $9,228. Lakini wanaotaka kujitenga wanasema maafisa wa usalama wa India ndio wamepanga mashambulizi haya ili kutisha watu wa Kashmiri wanaotaka kujitenga na India.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Wanaume katika jimbo hilo pia wametengeneza makundi ya kulinda usalama na wakati mwingine kumetokea maafa. Mwanamume wa miaka 70 aliuawa baada ya kudhaniwa yeye ni mmoja wa wale wanaowakata wanawake nywele. Watalii sita, mmoja kutoka Uingereza pia walitishiwa na kikundi kimoja eneo la Srinagar.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Waseem Ahmad alipigwa na kuumizwa na kundi la vijana kaskazini mwa Kashmir kwa sababu walishuku yeye ni mmoja wa washambulizi. Anasema walijaribu kumchoma akiwa hai lakini polisi walimwokoa.

Chanzo cha picha, Abid Bhat

Mzee huyu ambaye hakutaka kujulikana aliweka kamera za CCTV nyumbani kwake baada ya nywele za mke wa mtoto wake kukatwa mara mbili kwa muda wa siku tatu.

Abid Bhat ni mpiga picha anayeishi Srinagar.