Wahamiaji waliokwama Libya kusaidiwa kurudi makwao

Wahamiaji wanarudishwa Libya baada ya kukamatwa Tripoli, Libya 4 Novemba2017 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wahamiaji huwekwa vizuizini wanapofika Libya na kushindwa kwenda Ulaya

Mpango wa haraka wa uhamisho umeandaliwa kwa wahamiaji wanaokabiliwa na unyanyasaji katika vizuizi nchini Libya.

Ni mpango uliotolewa katika mkutano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya nchini Ivory Coast

Utawala wa Libya, unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ulijiunga na mkataba huo, lakini una udhibiti mdogo tu na kuna maswali kuhusu jinsi itakavyokuwa.

Wahamiaji watarudishwa kwao nyumbani.

Hatua hii ni baada ya video zinazoonyesha wahamiaji kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wakiuzwa nchini Libya kama watumwa, kuchapishwa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliita minada hiyo ya watumwa "uhalifu dhidi ya binadamu".

Mamia ya maelfu ya wahamiaji wamevuka jangwa la Sahara na bahari ya Mediterranean wakijaribu kufikia Ulaya.

Maelfu hufa katika safari hii na wale walioweza kufika Libya hawana pesa zozote na hii huwafanya wawe katika hatari mikononi mwa wafanyabiashara wa kisasa wa watumwa.

Libya ilianzisha uchunguzi rasmi kuhusu wahamiaji kuuzwa kama wafanyakazi wa shamba kwa kiasi cha dola 400 (£ 300) baada ya CNN kuchapisha picha za mnada wa watumwa mwezi Novemba.

Wahamiaji waliokolewa baada ya kuzuiliwa nchini Libya wamesema vizuizi hivyo ni "kama kuzimu"

Akizungumza huko Abidjan, Bwana Macron alisema "operesheni ya dharura"imekubaliwa na nchi tisa, ikiwa ni pamoja na Libya, Ufaransa, Ujerumani, Chad na Niger.

Libya imesisitiza makubaliano yake "kutambua makambi ambayo matukio hayo yanaendelea", alisema kwa mujibu wa shirika la habari la AFP

Waziri Mkuu wa Libya Fayez Sarraj amekubali kutoa idhini kwa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kutembelea makambi, jambo ambalo litawapa wahamiaji fursa ya kuhamishwa katika siku zijazo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sera za EU za kuilipa Libya ili iwazuie wahamiaji wanaotaka kwenda Ulaya, zimekashifiwa

Lakini AU na UN zimeshutumu Umoja wa Ulaya, EU kwa kuchangia katika unyanyasaji wa wahamiaji nchini Libya kupitia sera zao za kuzuia wahamiaji wa Libya kuingia Ulaya.