Trump na Urusi: Mshauri wa zamani Michael Flynn akiri kuwahadaa FBI

Michael Flynn arrives at Washington court for hearing on 1 Dec 2017

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Michael Flynn akiwasili Washington

Aliyekuwa mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa taifa wa Donald Trump, Michael Flynn, amekiri kwamba aliandikisha taarifa ya uongo kwa idara ya uchunguzi wa jinai ya Marekani, FBI, mwezi Januari.

Bw Flynn alishurutishwa kujiuzulu mwezi mmoja baada yake kupotosha ikulu ya White House kuhusu mkutano wake na balozi wa Urusi kabla ya Trump kuingia madarakani.

Mashtaka dhidi yake yaliwasilishwa na mwanasheria maalum Robert Mueller kama sehemu ya uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani wa 2016.

Bw Flynn alifika mahakamani Ijumaa.

Alikiri kosa moja ya kutoa makusudi "taarifa za uongo, za kubuni na za kupotosha".

Kwa mujibu wa mwanahabari wa AFP, Bw Flynn aliulizwa na Jaji Rudolph Contreras iwapo alitaka kukiri makosa hayo na akajibu kwa kusema "Ndio".

Jaji aliendelea: "Nakubali kukiri kwako makosa. Hivyo hakutakuwa na kusikizwa kwa kesi na labda huenda kusiwe na rufaa."

Alijisalimisha kwa FBI kabla ya kufanyika kwa kikao cha mahakama Ijumaa asubuhi mjini Washington DC.

Msaidizi huyo wa zamani wa Trump ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi katika utawala wa Trumpa ambaye amepatikana na hatia katika uchunguzi huo unaoendeshwa na Mueller.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Michael Flynn alijiuzulu Februari

Oktoba, meneja wa zamani wa kampeni za urais wa Trump, Paul Manafort, alituhumiwa kula njama ya kuilaghai Marekani katika shughuli za kibiashara na Ukraine.

Aidha, iliibuka kwamba msaidizi mwingine wa zamani, George Papadopoulos, amekiri makosa ya kutoa taarifa za uongo kwa maajenti wa FBI.