Kiongozi wa mikakati wa upinzani Kenya David Ndii akamatwa

David Ndii Haki miliki ya picha NASA Coalition/Twitter

Mmoja wa wakuu wa mikakati wa muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) a likamatwana kuzuiliwa na polisi siku chache baada ya kuteuliwa kuongoza moja ya makundi ya muungano huo.

Bw David Ndii, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, alikuwa ameteuliwa kuongoza Kamati ya Taifa ya kusimamia Mabunge ya Wananchi.

Mabunge hayo ya wananchi yaliundwa na Nasa, chini ya waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, kama njia ya kushinikiza mageuzi nchini humo baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao Bw Odinga na muungano wake walisusia.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini Kenya Keriako Tobiko baadaye aliagiza polisi wamwachilie huru Bw Ndii kwa dhaama ya polisi.

Aidha, aliwataka polisi kufanya uchunguzi na faili ya matokeo ya uchunguzi huo kuwasilishwa kwake kwa hatua zaidi.

Bw Ndii alikamatwa Jumapili jioni akiwa kwenye hoteli moja jimbo la Kwale pwani ya Kenya.

Mkewe, Mwende Gatabaki, akiwahutubia wanahabari, mapema Jumatatu alikuwa amesema mumewe alikamatwa na wanaume saba ambao walimfahamisha kwamba angepelekwa kito cha polisi cha Diani lakini walipofika huko hawakumpata.

"Walikuwa wanatudanganya, kama watoto," alisema.

Kadhalika, walitaka kuingia kwenye chumba chao hotelini kufanya ukaguzi lakini alipowauliza kibali cha kufanya upekuzi wakasema hawakuhitaji kibali hicho kwa sababu walikuwa wakuu wa kituo cha polisi.

Aidha, walikuwa wanatafuta kompyuta ambazo Bi Gatabaki anasema hawakuwa nazo chumbani.

Amesema polisi hawakueleza sababu ya kukamatwa kwake na kwamba alipozidi kuuliza maswali kuhusu alipokuwa mumewe naye alikamatwa na kuzuiliwa kwa muda.

Bi Gatabaki amesema familia hiyo ilikuwa likizoni Kwale na pia kwa ajili ya kuhudhuria harusi ya mpwa wao.

Upinzani umeshutumu hatua ya polisi ya kumkamata na kumzuilia Bw Ndii.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, ambaye ni mwanachama wa muungano wa Nasa, alikuwa amesema polisi waliwafahamisha kwamba mwanamikakati huyo angeshtakiwa kwa tuhuma za uchochezi.

"Mashtaka hayo yanahusiana na maneno aliyoyatamka miezi mingi iliyopita. Kawaida, walifaa kumuita kwa mahojiano na si kumvamia akiwa likizoni," amenukuliwa na kituo cha habari cha NTV.

Bw Ndii alifikishwa katika majengo ya mahakama Milimani lakini kabla ya kufunguliwa mashtaka, Bw Tobiko akaagiza aachiliwe kwa dhamana.

Bw Ndii ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Jubilee yake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto na huandika makala yanayochapishwa mwishoni mwa wiki katika moja ya magazeti makuu nchini humo.

Alizua utata alipopendekeza kwamba baadhi ya majimbo Kenya yanaweza kujitenga iwapo mabadiliko hayatafanikiwa katika siasa na uongozi nchini Kenya.

Muungano wa upinzani uliunda kundi la watu sita kuongoza Mabunge ya Wananchi huku ukiendelea na juhudi za kushinikiza mageuzi nchini humo.

Huwezi kusikiliza tena
Odinga asema naye ataapishwa kuiongoza Kenya

Bw Odinga alisema Mabunge ya Wananchi yatajumuisha wadau kutoka nyanja mbalimbali na yatatumiwa kutoa mwelekeo kwa nchi.

Wiki iliyopita, alidokeza kwamba mabunge hayo yatashirikishwa katika mpango wake wa kutaka kuapishwa kuwa kiongozi wa Kenya tarehe 12 Desemba.

Majimbo kumi kati ya 47 nchini Kenya, ambayo yana viongozi na wafuasi wengi wa upinzani, tayari yamepitisha hoja ya kuundwa kwa mabunge hayo.

Mada zinazohusiana