Kiongozi mwingine akiapishwa litakuwa kosa la uhaini Kenya

Raila Odinga Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raila Odinga

Mwanasheria mkuu wa Kenya Prof Githu Muigai amesema jaribio lolote la kumuapisha kiongozi mwingine wa Kenya litakuwa ni uhaini wa hali ya juu.

Prof Muigai amesema hayo huku kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga akisisitiza kwamba ataapishwa kuwa rais Jumanne wiki ijayo.

Bw Odinga alitangaza mwezi uliopita kwamba ataapishwa na Mabunge ya Wananchi ambayo yalipendekezwa na muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa).

Ingawa hakumtaja mtu yeyote, Prof Muigai, akiwahutubia wanahabari Nairobi, alisema shughuli hama hiyo ya kumuapisha kiongozi ambaye hajatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) haina msingi wowote kikatiba na kwamba itakuwa "bure na batili".

"Sheria za jinai za Jamhuri ya Kenya zinazungumzia shughuli kama hiyo kuwa uhaini wa hali ya juu," amesema.

"Wanaoshiriki watakuwa wanajihusisha katika uhaini wa hali ya juu, pamoja na wote wanaofanikisha shughuli kama hiyo."

Adhabu ya kosa la uhaini kwa mujibu wa sheria za Kenya ni kifo.

Prof Muigai amesema Mabunge ya Wananchi ambayo yanaundwa na Nasa pia ni kinyume cha sheria.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Kenyatta aliapishwa kwa muhula wa pili tarehe 28 Novemba

Kufikia sasa, mabunge 12 ya majimbo, ikiwa ni pamoja na Mombasa, ambayo yanaongozwa na magavana wa muungano wa Nasa tayari yamepitisha azimio la kuundwa kwa mabunge hayo ya wananchi.

Kenya kwa jumla ina majimbo 47.

Nasa ilipendekeza kuundwa kwa mabunge hayo kama njia ya kushinikiza mageuzi nchini humo baada ya kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 26 Oktoba.

Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo ambao ulisusiwa na upinzani.

Alipata kura 7.5 milioni, sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa ingawa waliojitokeza walikuwa asilimia 39.

Bw Kenyatta aliapishwa kuwa rais tarehe 28 Novemba kwenye sherehe ambayo upinzani ulisusia.

Huwezi kusikiliza tena
Odinga asema naye ataapishwa kuiongoza Kenya

Bw Odinga amesisitiza kwamba muungano wake hautambui ushindi wa Kenyatta na kwamba hautamtambua kama kiongozi halali wa nchi hiyo.

Marekani imemtaka Bw Odinga kuacha mpango huo wake wa kuapishwa kama rais wa nchi hiyo.

Waziri msaidizi wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika, Donald Yamamoto ambaye alikuwa amezuru Kenya alimtahadharisha Bw Odinga na pia akahimiza kuwepo mashauriano kati yake na serikali iliyopo madarakani.

Aidha alitahadharisha dhidi ya matendo ambayo yako nje ya katiba nchini humo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii