Korea Kusini yaiwekea vikwazo Korea Kaskazini

Korea Kusini yaiwekea vikwazo Korea Kaskazini
Image caption Korea Kusini yaiwekea vikwazo Korea Kaskazini

Korea Kusini imetangaza vikwazo vipya dhidi ya mashirika 20 mengine ya Korea Kaskazini, na watu kadha, ili kujibu jaribio la kombora pamoja na mradi wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Wizara ya fedha ilisema hatua hizo zinalenga kuzuia fedha kugharamia mradi wa silaha, kinyume cha sheria.

Karibu mashirika na watu hao wote, yamo katika sekta za benki na safari za meli, na tayari yamepigwa marufuku na Marekani.

Hatua hiyo inachukuliwa majuma mawili baada ya Korea Kaskazini kufanya majaribio ya kufyatua kombora ambalo linasemekana linaweza kufika pahala popote pale nchini Marekani.

Kombora hilo kwa jina Hwasong-15 ambalo imesema ndio kombora lenye uwezo mkubwa lilirushwa katika giza mapema siku ya Jumatano.

Lilianguka katika maji ya Japan lakini liliweza kuruka juu zaidi ya kombora jingine lolote la taifa hilo .

Kitengo cha habari cha taifa hilo KCNA kilisema kuwa kombora hilo liliruka katika kimo cha kilomita 4,475 na kusafiri kwa umbali wa kilomita 950 katika dakika 53.

Mada zinazohusiana