Bomu la Korea Kaskazini bado linatetemesha ardhi tangu Septemba

North Korea's Rodong Sinmun newspaper showed a picture of Kim Jong-Un inspecting the purported nuclear warhead Haki miliki ya picha Rodong Sinmun
Image caption Korea Kaskazini imesisitiza kwamba ina haki ya kustawisha silaha za nyuklia

Korea Kaskazini ilipofanyia majaribio bomu lake la nyuklia Septemba, bomu hilo lilisababisha mitetemeko kadha midogo ya ardhi pamoja na tetemeko kubwa la ardhi la nguvu ya 6.3 kwenye vipimo vya Richter.

Mitetemeko ya baada ya tetemeko kubwa la ardhi imeendelea kutokea eneo hilo.

Jumamosi, Idara ya Jiolojia ya Marekani inasema mitetemeko mingine miwili midogo ya ardhi ilitokea.

Hilo limezua mjadala kuhusu nini kinatokea chini ya ardhi katika eneo ambapo kulitekelezwa jaribio hilo la bomu.

Nini kilitokea wakati wa jaribio lenyewe?

Mnamo 3 Septemba, Korea Kaskazini ilifanyia majaribio bomu lake la nyuklia lenye nguvu zaidi katika eneo la kujaribia mabomu na silaha Punggye-ri eneo lenye milima kaskazini magharibi mwa taifa hilo.

Pyongyang ilisema bomu hiyo lilikuwa la haidrojeni, jambo ambalo lingelifanya kuwa na uwezo mara nyingi zaidi kuliko bomu la kawaida la atomiki.

Wataalamu wameeleza wasiwasi kwamba mlipuko wa bomu hilo ulikuwa na nguvu sana kiasi kwamba huenda ulidhoofisha msingi wa milima iliyopo karibu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Majaribio yote ya silaha za nyuklia yamefanyika Punggye-ri chini ya ardhi

Mbona kuna mitetetemeko mpaka sasa?

Kwa mujibu wa taasisi ya jiolojia ya Marekani, USGS, mitetemeko iliyotokea wikendi ilikuwa "matukio ya kulegeza au kupunguza" shinikizo.

Mitetemeko hiyo ilikuwa na nguvu ya 2.9 na 2.4.

"Unapokuwa na jaribio kubwa la nyuklia, sehemu ya juu a ardhi husonga eneo hilo, na huchukua muda kabla ya kila kitu kutulia tena. Tumekuwa na mitetemeko kadha tangu kutekelezwa kwa jaribio hilo la sita la nyuklia," afisa aliambia Reuters.

Kusonga huko kwa sehemu ya juu ya uso wa dunia inaendana sambamba na inavyotokea mitetemeko ya ardhi.

Wanasayansi wanasema hiyo hutarajiwa kutokea wiki kadha au miezi kadha baada ya mlipuko mkubwa wa aina hiyo.

"Mitetemeko hii midogo baada ya jaribio la bomu la nyuklia lililosababisha tetemeko la ardhi ya nguvu ya 6.3 si jambo la kushangaza," anasema Dkt Jascha Polet, mtaalamu wa mitetemeko ya ardhi na jiolojia ambaye ni profesa katika chuo kikuu cha mafunzo anuwai cha jimbo la California, alipozungumza na BBC.

Baada ya tetemeko kubwa la aina hiyo, mitetemeko midogo ambayo huenda ikipunguza nguvu zake ni kawaida, mawe na miamba inapohama na kupunguza shinikizo.

Maeneo yaliyo karibu na eneo kunakofanyika majaribio haya "hubadilishwa maumbile yake, na hili husababisha kuongezeka na pia kupunguka kwa shinikizo, jambo ambalo huathiri kuenea kwa mitetemeko midogo ya baada ya tetemeko kubwa," anasema Bi Polet.

"Hali kwamba chanzo cha tetemeko lenyewe ni mlipuko haibadili jinsi tunavyotarajia nguvu au nishati kwenye uso wa dunia zianze kujitandaza tena," mtaalamu mwingine wa jiolojia ambaye pia huangazia mikasa Mika McKinnon, aliambia BBC.

Lakini utafiti wa milipuko ya nguvu sawa na uliotokea baada ya jaribio la bomu la Korea Kaskazini katika eneo la majaribio ya mabomu ya nyuklia Nevada, ambapo Marekani ilifanyia majaribio mengi kwa miongo kadha, umegundua kwamba mitetemeko ya baada ya tetemeko kuu iliyotokea ilikuwa michache na ya nguvu za chini kuliko iliyoshuhudiwa Korea Kaskazini.

Kwa hivyo, kila eneo ni pekee kivyake.

Mitetemeko inaweza kuharibu kabisa eneo?

Moja ya yaliyodhaniwa yangefanyika baada ya jaribio hilo la Septemba ni kwamba njia za chini kwa chini ambazo zilikuwa zimechimbwa kwenye milima eneo hilo ili bomu lilipuliwe ndani chini ya ardhi zingeporomoka.

"Unapoweka nguvu nyingi ndani ya eneo moja, ndivyo eneo hilo linavyokuwa dhaifu," Mika McKinnon anasema.

"Kadiri majaribio zaidi yanavyotekelezwa, ndivyo kunavyokuwa na nguvu zaidi, na njia ya kutandaza tena shinikizo kwenye mawe na ndivyo miamba zaidi itakavyovunjika."

Kumekuwa na ishara kwamba huenda baadhi ya njia za chini kwa chini ziliporomoka, anasema.

"Dalili za mitetemeko ambayo inaonekana huenda ilisababishwa na kuanguka kwa miamba zimesikika. Mitetemeko hii itatokea zaidi na zaidi."

Lakini anaongeza kwamba hakuna njia yoyote ya kujua iwapo mfumo wote wa njia za chini kwa chini utaporomoka na kwamba hilo ni tatizo la kihandisi badala ya kuwa la kisayansi.

Haifahamiki iwapo shughuli hii tayari imedhoofisha sana eneo hilo la kujaribia silaha kiasi cha kutoweza kutumika tena, lakini Korea Kaskazini imetoa viashiria kwamba majaribio yake yajayo ya silaha za nyuklia yatakuwa juu ya ardhi.

Kunaweza kutokea mlipuko wa volkano?

Karibu na eneo la majaribio la Punggye-ri kuna mlima wa volkano ulio hai wa Paektu, mlima ambao huchukuliwa kuwa mtakatifu Korea Kaskazini.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kim Jong-un anaonekana kufurahi akiwa juu ya Mlima Paektu

"Mitikisiko inagonga volkano hiyo na kufikia matope ya moto yaliyo chini ya volkano hiyo," anasema Bi McKinnon.

Lakini anasema ni "vigumu sana kwamba baadhi ya nguvu za mitetemeko hiyo zinaweza kuwa za kutosha kuifanya volkano hiyo ilipuke."

Volkano hiyo ililipuka mara ya mwisho 1903, lakini majaribio ya bomu hiyo la Septemba yaliibua wasiwasi kwamba mitetemeko hiyo huenda ikasababisha mlima huo ulipuke tena.

Kumekuwa na mjadala mkali, lakini hakuna takwimu za kuthibitisha uwezekano huo.

Utafiti ambao matokeo yake yalichapishwa jarida la Nature mwaka jana uliobashiri kwamba mawimbi ya mitikisiko kutoka kwa jaribio la nyuklia linalosababisha tetemeko la ardhi la nguvu ya 7.0 yanaweza kusababisha "mabadiliko katika shinikizo" ambayo yanaweza kuwa na madhara.

Lakini Bi Polet anasema, "kuna ufahamu mdogo sana kuhusu kile kinachoweza au kisichoweza kusababisha mlipuko wa volkano" na hakuonekani kuwa na ushahidi wowote uliothibitishwa wa kuonesha uhusiano kati ya majaribio ya mabomu ya nyuklia yaliyotekelezwa Nevada na shughuli za volkano maeneo ya karibu kama vile Timber Mountain na Long Valley Caldera.

Hakujakuwa na shughuli zozote za volkano zilizoripotiwa kutokana na majaribio ya silaha za nyuklia katika visiwa vyenye shughuli nyingi za volkano vya Aleutian.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un pia anaonekana kuwa na imani sana na mlima huo mtakatifu.

Kwa mujibu wa Reuters, vyombo rasmi vya Korea Kaskazini vimeripoti kwamba Kim alikwea mlima huo wa volkano Jumamosi akiwa pamoja na maafisa wengine wakuu serikali "kusisitiza ruwaza yake ya kijeshi".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii