Kenyatta awaonya wanaotishia mfumo wa kikatiba Kenya

Rais Kenyatta Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta/Facebook

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amewaonya wapinzani wake dhidi ya kutishia mfumo uliowekwa kikatiba.

Akihutubu wakati wa maadhimisho wa sikukuu ya Jamhuri jijini Nairobi, Rais huyo amesema: "yeyote atakayeharibu mali, anayeamua kutumia fujo zisizo na maana badala ya kutumia mifumo ya kikatiba, wote hawa ni maadui wa jamhuri, na hivyo ndivyo watachukuliwa."

Bw Kenyatta alionekana kana kwamba anazungumza kuhusu muungano mkuu wa upinzani National Super Alliance (Nasa) na kiongozi wao Raila Odinga.

Muungano huo umekuwa ukiandaa maandamano mara kwa mara kushinikiza mageuzi katika mfumo wa kisiasa nchini humo na tume ya uchaguzi.

Waandamanaji wa muungano huo wamekuwa wakikabiliana na polisi na vifo na uharibifu wa mali hutokea.

"Nilipokula kiapo 2013, na nikarudia tena mwezi uliopita, Wakenya walinipa vifaa viwili vya mamlaka. Moja ni Katiba; na pili upanga. Niliapa kuvitumia kuilinda na kuikinga Kenya dhidi ya aina zozote za hatari, kutoka ndani na nje.

"Ndio maana nina wajibu wa kuwatumikia kama Rais, na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yetu ya Ulinzi. Sitakosa kutimiza matarajio yenu.

"Leo nawatahadharisha wale wanaopuuza mfumo wetu wa kikatiba. Katiba na nia ya jumla ya watu wote. Hakuna aliye juu: bila kujali wewe ni nani, wewe uko chini yake. Chochote kilicho nje ya katiba ni uchokozi."

Bw Odinga alikuwa ameahidi kuwa angeapishwa leo na Mabunge ya Wananchi kuiongoza Kenya.

Sherehe hiyo hata hivyo iliahirishwa kwa muda usiojulikana na muungano wa Nasa.

Mwanasheria mkuu Githu Muigai alikuwa ametahadharisha kuwa hatua ya kumuapisha kiongozi mwingine ingekuwa uhaini wa kiwango cha juu.

Aidha, alisema Mabunge ya Wananchi ambayo yanaundwa na muungano huo wa upinzani ni kinyume cha sheria na kutahadharisha serikali za kaunti dhidi ya kutumia fedha za umma katika mpango huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii