Erdogan: Mataifa yanafaa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Wapalestina

Turkish President Recep Tayyip Erdogan address the meeting of the Organisation for Islamic Cooperation in Istanbul on Wednesday Haki miliki ya picha TR
Image caption Recep Tayyip Erdogan amesema hatua ya Marekani ni haramu na inachochea zaidi ugaidi

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameyahimiza mataifa ya Kiislamu kuutambua mji wa Jerusalem kama "mji mkuu wa taifa la Wapalestina unaokaliwa na taifa jingine".

Akihutubia mkutano mkuu wa muungano wa nchi za Kiislamu (OIC), amesema hatua ya Marekani ya kuutambua mji huo kama mji mkuu wa Israel ni "batili".

Msimamo wake umeungwa mkono na mataifa 57 yaliyohudhuria mkutano huo, kwenye taarifa ya pamoja.

Bw Erdogan pia kwa mara nyingine ameishutumu Israel na kuiita "taifa la kigaidi".

KIongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Marekani "imejiondoa kutoka kwa kuwa mhusika mkuu katika shughuli ya kutafuta amani".

"Hatutakubali mchango wowote wa Marekani katika shughuli ya kutafuta amani. Wamethibitisha kikamilifu kwamba wanaipendelea Israel," ameuambia mkutano huo.

Hadhi ya mji wa Jerusalem imekuwa sehemu ya mzozo wa Waisraeli na Wapalestina.

Kwa nini Jerusalem inazozaniwa?

Mji huo una maeneo matakatifu ya dini tatu zenye kufuata imani ya Ibrahim - Uyahudi, Ukristo na Uislamu - sana maeneo mengi yanapatikana Jerusalem Mashariki.

Israel ilitwaa eneo hilo kutoka Jordan wakati wa vita kati ya nchi za Kiarabu na Israel mwaka 1967 na imekuwa ikiuchukulia mji wote kuwa mji wake mkuu ambao hauwezi kugawanywa.

Jerusalem Mashariki hutazamwa kuwa mji mkuu wa taifa la Wapalestina (litakapoundwa) na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu pamoja na Wapalestina wenyewe.

Kwa mujibu wa maafikiano wakati wa mazungumzo ya amani ya Wapalestina na Waisraeli ya 1993, hatima ya mji huo ilifaa kuamuliwa wakati wa hatua za mwisho za mazungumzo.

Hatua ya Israel kudhibiti Jerusalem yote haijawahi kutambuliwa kimataifa na nchi zote zina afisi za kibalozi Tel Aviv.

Tangu 1967, Israel imejenga makazi kadha ya Wayahudi na kuna takriban walowezi 200,000 wa Kiyahudi eneo hilo. Makazi haya yamekuwa yakishutumiwa na jamii ya kimataifa.

'Suluhu ya kidiplomasia'

Mwandishi wa BBC Mark Lowen aliyepo Istanbul anasema hotuba zilizotolewa katika mkutano huo wa OIC zilikuwa kali.

Lakini swali kuu ni hatua zinazoweza kuchukuliwa na muungano huo, ikizingatiwa kwamba baadhi ya nchi za Kiislamu wanachama wa muungano huo humuunga mkono sana Trump kushinda baadhi ya nchi.

Mwandishi wetu anasema baadhi ya nchi zimewatuma tu mawaziri katika mkutano huo, ishara pengine ya matarajio yake kutoka kwa mkutano huo.

Maandamano katika baadhi ya nchi za Kiislamu kuhusu mzozo huo wa Jerusalem pia hayajakuwa makubwa sana katika baadhi ya nchi.

Bw Erdogan alitishia kuvunja uhusiano kati ya Uturuki na Israel kabla ya tangazo la bw Trump wiki iliyopita, lakini hakueleza nia yoyote ya kufanya hivyo wakati wa hotuba yake.

Uturuki na Israel walifufua uhusiano wa kibalozi 2016, miaka sita baada ya Uturuki kukatiza uhusiano kulalamikia kuuawa kwa wanaharakati tisa wa Uturuki ambao waliuawa katika makabiliano na makomando wa Israel kwenye meli iliyokuwa inajaribu kukiuka marufuku ya Israel baharini ya kutosafirisha misaada kuingia Gaza.

Bw Erdogan badala yake alihimiza kuwepo kwa hatua za pamoja kutoka kwa nchi za Kiislamu dhidi ya hatua hiyo ya Bw Trump kuhusu Jerusalem.

"Nayakaribisha mataifa yote yanayoithamini sheria ya kimataifa na haki kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa taifa la Palestina unaokaliwa na taifa jingine," alisema.

"Wale wanaopigana na marafiki zao husahau kupigana na maadui zao," aliongeza.

"Tunahitaji suluhu ya kidiplomasia. Lazima tuizuie Israel isichukua ardhi zaidi na zaidi kutoka kwa Palestina siku baada ya siku. Na hatufai kukubali sera na mtazamo ambao Israel imekuwa ikionesha siku baada ya siku."

Kwa nini Trump akafanya hivyo?

Rais Trump alisema kwamba "ameamua ni wakati mwafaka kutambua rasmi Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel."

"Nimeamua hatua hii itakuwa ndiyo bora zaidi kwa maslahi ya Marekani katika juhudi za kutafuta amani kati ya Waisraeli na Wapalestina," alisema.

Alisema ameiagiza wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuanza kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.

Licha ya onyo kwamba hatua kama hiyo inaweza kuzua wimbi la machafuko kanda ya Mashariki ya Kati, hatua hiyo inatimiza ahadi aliyoitoa Trump wakati wa kampeni na pia kuwafurahisha wafuasi wenye msimamo mkali wa Bw Trump.

Bw Trump alisema kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel ilikuwa "ni kutambua uhalisia tu," na akaongeza kwamba "ndiyo hatua ya busara kuichukua."

Bw Trump alisema Marekani itaendelea kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili - taifa la Waisraeli na Wapalestina - mataifa yote yakiishi pamoja kwa amani.

Rais huyo pia alijizuia kurejelea msimamo wa Israel kwamba Jerusalem ni mji wake mkuu wa milele ambao hauwezi kugawanywa.

Wapalestina wanataka Jerusalem Mashariki iwe mji mkuu wa taifa la Wapalestina litakapoundwa.

Kuuhamisha ubalozi

Kando na kuitambua Jerusalem, Rais Trump alisema pia kwamba meagiza wizara ya mambo ya nje ya Marekani kujiandaa kuuhamisha ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.

Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa mara ya pili Jumatatu alishutumu uamuzi wa Trump wa kuhamisha ubalozi wa Marekani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji mjini Beirut wakipinga hatua ya Trump

Akizungumza Ankara, Uturuki baada ya mazungumzo na mwenzake Recep Tayyip Erdogan, Bw Putin alisema:

"Urusi na Uturuki wanaamini uamuzi wa Marekani wa kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na kuhamisha ubalozi wa Marekani huko hautasaidia kupatikana kwa suluhu ya mzozo Mashariki ya Kati."

"Kimsingi, hii inaweza kufuta matumaini ya shughuli ya kutafuta amani ya Wapalestina na Waisraeli."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii