Mfumo wa sayari unaofanana na wetu wagunduliwa

Kepler-90 Haki miliki ya picha NASA
Image caption Mchoro: Mfumo wa sayari wa Kepler-90 ndio wa kwanza kufanana na mfumo wetu wa jua kwa idadi ya sayari

Shirika la anga za juu la Marekani Nasa limegundua nyota ambayo inazungukwa na sayari nane, sawa na mfumo wetu wa jua ambao una sayari nane.

Hiyo ndiyo idadi ya juu zaidi ya sayari kugunduiwa zikiizunguka nyota nje ya mfumo wetu wa sayari.

Nyota hiyo iliyopewa jina Kepler-90, ina joto kiasi na ni kubwa kidogo kulishinda Jua.

Awali, wataalamu wa anga za juu walikuwa wamefahamu uwepo wa sayari saba pekee zilizokuwa zinaizunguka.

Lakini sasa wanasayansi wa Nasa wanasema wamegundua uwepo wa sayari nyingine ndogo iliyojaa mawe.

"Hii inaifanya Kepler-90 kuwa nyota ya kwanza kuwa na sayari nyingi sawa na za Mfumo wa Jua," anasema Christopher Shallue, mhandisi wa masuala ya programu za kompyuta katika Google, kampuni ambayo ilichangia katika ugunduzi huo.

Wahandisi kutoka kwa Google walitumia mashine yenye uwezo wa kufikiria kutafuta sayari ambazo zilikuwa awali hazionekani kwa teknolojia za awali.

Haki miliki ya picha NASA
Image caption Kulinganisha Kepler-90 na Mfumo wetu wa Jua
Haki miliki ya picha NASA
Image caption Mchoro: Darubini ya Kepler ilitumiwa kugundua mfumo huo wa jua na sayari zake

Ugunduzi huo ulifanywa kwa kutumia darubini maalum ya Nasa ya kutazama yaliyomo anga za juu ya Kepler.

Nyota hiyo inapatikana mbali sana, miaka 2,545 kwa kasi ya kusafiri kwa mwanga.

Lakini mpangilio wake wa sayari unaonekana kufanana na wetu sana.

Andrew Vanderburg, aliyeshiriki katika ugunduzi huo katika Chuo Kikuu cha Texas, Austin, alisema: "Mfumo wa nyota wa Kepler-90 ni kama mfano mdogo wa mfumo wetu wa jua. Una sayari ndogo zinazozunguka kwa ndani na zile kubwa zikiwa nje kidogo, lakini kila kitu kimepangwa kwa karibu sana."

Ili kufahamu ukaribu wa sayari hizo kwa nyota hiyo, mzingo wa sayari iliyo nje zaidi ni umbali sawa na wa Dunia kutoka kwa Jua.

Kwa sababu sayari inayofanana na Dunia kwenye mfumo huo, ambayo imepewa jina Kepler-90i, inapatikana ndani sana - humaliza mzunguko mmoja kwenye nyota hiyo kwa kutumia siku 14.4 pekee.

Inakadiriwa kwamba sayari hiyo ina joto sana, karibu nyuzi joto 425C.

Teknolojia hiyo mpya ya kutumia mashine zenye uwezo wa kufikiria ilitumiwa pia kugundua sayari nyingine yenye ukubwa sawa na Dunia ambayo imepewa jina Kepler 80g, na inazunguka nyota nyingine.

Inakadiriwa kwamba kuna sayari takriban 3,500 zinazozunguka nyota mbalimbali, nyingi ambazo zimegunduliwa katika miongo ya karibuni.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii