Mjadala wasitishwa baada wanajeshi 'kuingia' bungeni Uganda

Spika wa bunge nchini Uganda Rebecca Kadaga Haki miliki ya picha facebook
Image caption Spika wa bunge nchini Uganda Rebecca Kadaga

Spika wa bunge la Uganda, Rebecca Kadaga amelazimika kusimamisha mjadala wa muswada tata uliokusudia kufuta kipengele cha ukomo wa umri wa rais baada ya mbunge wa upinzani Lucy Akello kulalamika kuwa kulikuwa na wanajeshi kwenye moja ya kumbi za bunge inayotumika kufanya ibada.

Mwandishi wa BBC Patience Atuhaire, anaelezea kuwa baadhi ya wabunge waliorudi kutoka kuchunguza ukumbi huo walisema kuwa walipata chupa zenye mikojo, ambazo wanajeshi hao walikuwa wanatumia kujisaidia.

Walisema pia wamepata vyombo vilivyotumika na mabaki ya chakula.

Baadhi ya wabunge walijaribu kuvipeleka vyombo hivyo bungeni kabla ya kipindi kuanza lakini maafisa wa usalama walivinyakua.

Mwandishi wa BBC Patience Atuhaire anasema, hali ni ya taharuki ndani ya ukumbi wa bunge na mhemko ni mkubwa wakati wabunge wanaposema maeneo yao ya ibada yamedharauliwa

Kumbi zote za ibada za Wakatoliki na Waprotestanti zinaelezwa kutumika na wanajeshi.

Kisa hicho kiliwashutua raia wangi wa Uganda.

Maafisa wa polisi na wale wa kijeshi wamepelekwa nje ya bunge pamoja na maeneo mengine ya mji .

Mamlaka inasema kuwa wamejiandaa dhidi ya ghasia wakati wa mjadala.

Bunge linatarajiwa kuendelea siku ya Jumanne mchana.Wakati wa makabiliano kati ya wabunge wa upinzani mnamo mwezi Septemba , wanajeshi kutoka katika kikosi maalum waliokuwa wamevalia sare za raia waliingia katika bungeni na kuanza kuwapiga na kuwakamata wabunge.

Mada zinazohusiana