Marafiki wa Korea Kaskazini wafichuliwa

Rais Kim Jong un wa Korea Kaskazini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Kim Jong un wa Korea Kaskazini

Taifa la Korea Kaskazini huonekana kana kwamba limetengwa na ulimwengu , lakini ukweli ni kwamba lina uhusiani wa kidiplomasia na mataifa takriban 50.

Ni mataifa gani hayo? Na uhusiano wao ukoje?.

Taifa la Korea Kaskazini linaendelea kuonekana taifa baya kila uchao.

Lakini licha ya kutengwa linaendelea kuwa na uhusiano mkubwa wa kidiplomasia na mataifa mengi.

Tangu kuanzishwa kwa taifa la Korea Kaskazini 1948, taifa hilo limefanikiwa kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na zaidi ya mataifa 160 huku likiwa na balozi 55 na afisi ndogo za mabalozi katika mataifa 48.

Kati ya mataifa hayo ,25 yana ubalozi ndani ya taifa la Korea Kaskazini ikiwemo Uingereza, Ujerumani na Sweden kama ilivyoangaziwa na taasisi ya Lowy Institute.

China na Urusi ambayo ndio majirani zake wa kikomyunisti walikuwa wa kwanza kuweka uhusiano wa kidiplomasia baada ya kubuniwa kwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Korea kama ilivyojulikana rasmi.

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha,

Rangi ya machugwa inawakilisha mataifa yenye ubalozi wa Korea Kaskazini na yana ubalozi Korea Kaskazini. Rangi ya kijani inawakilisha mataifa yenye ubalozi wa Korea Kaskazini lakini hayana ubalozi nchini Korea Kaskazini

Lakini Marekani sasa inajaribu kuushawishi ulimwengu kukatiza uhusiano wake na Pyongyang huku mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley akiyataka mataifa yote kukatiza uhusiano na taifa hilo.

Miongoni mwa mataifa yale yanayotarajiwa kuchukua hatua hiyo ni Uhispania ,kuwait, Peru, Mexico, Italy na Myanmar ambayo pia inajulikana kama Burma ,mataifa ambayo yamewaondosha mabalozi wake katika kipindi cha miezi michache iliopita.

Ureno, Uganda, Singapore,UAE na Ufilipino pia yamesitisha uhusiano ama hata kukata uhusiano mwengine.

Lakini balozi nyingi za Korea Kaskazini duniani, na zile zilizopo katika taifa hilo zitaendelea kuwa wazi kwa biashara.

Mataifa mengine yameonekana kuimarisha uhusiano wao na Pyonyang ikiwemo mataifa ya Afrika yakishirikiana na taifa hilo katika miradi ya ujenzi mbali na mazungumzo kuhusu kawi na kilimo.

Lakini uhusiano wa kidiplomasia na Korea Kaskazini umezorota.

Ni mataifa sita kati ya 35 , mwanachama wa shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD,mataifa yenye uwezo mkubwa duniani ambayo bado yana balozi zake nchini Korea Kaskazini.

Marekani haijawahi kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Korea Kaskazini.

Mataifa mengine ambayo hayajawahi kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Korea Kaskazini ni Japan na Korea Kusini.

Hatua hii inamaanisha kwamba kwamba Marekani pamoja na washirika wake wa karibu wa bara Asia wanategemea mataifa mengine ili kuweza kupata habari chache zinazotoka Pyonyang.

Habari hizo hutoka katika mataifa kama vile Ujerumani, Uingereza, Sweden ambayo yako katika eneo moja na ambayo yameshindwa kufunga balozi zao nchini humo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Korea Kaskazini husherehekea makombora yake iliofanyia majaribio kwa kupiga muhuri

Uhusiano wa kidiplomasia wa Korea Kaskazini barani Asia, Ulaya ,Mashariki ya kati na Afrika ni muhimu katika kujipatia kipato kwa njia za halali na haramu mbali na kukwepa mtego wa Umoja wa Mataifa na vikwazo visivyoisha.

Balozi hizo hujifadhili zenyewe na madai kwamba zinatekeleza operesheni kufanya biashara haramu zipo.

Mataifa ya Ulaya yenye balozi za Korea Kaskazini yamelalamika kwamba majengo ya balozizao yamekuwa yakikodishiwa wafanyibiashara wa nyumbani.

Nchini Pakistan ,taifa ambalo lina historia ya kutii Pyonyang, wizi uliofanyika katika nyumba ya balozi wa Korea Kaskazini ulizua shauku kwamba huenda alikuwa akiuza pombe ya hali ya juu.

Katika pande zote, vitengo vya ujasusi haviaminiani.

Huwachunguza mabalozi na kuwawekea vikwazo vikali vya usafiri.

Korea Kaskazini pia huchunguza kwa karibu vitendo vya mabalozi wake, ikihofia kwamba huenda wakahamia mataifa mengine.

Mbali na hayo yote, swali kuu ni je diplomasia inaweza kusaidia kivipi?

Kwa mataifa yenye jamii za kikomyunisti kama vile Cuba, Venezuela na Laos, uhusiano na Korea Kaskazini unaleta mfano wa usaidizi wa mataifa yenye maono ya kufanana.

Lakini siku hizi ,uhusiano huo husababishwa na msimamo dhidi ya sera za Marekani ikilinganishwa na maono sawa kama yalivyofanya mataifa ya Syria na Iran.

Kila habari zinazochapishwa dhidi ya Pyongyang, mabalozi wa taifa hilo hutakiwa kuunga mkono taifa lao na kutoa matamshi machafu dhidi ya maadui zao.

Hatua nyengine kama hizo hupewa umuhimu mkubwa , kwa mfano vinyozi waliokosoa mtindo wa nywele za rais Kim Jong Un.

Mataifa ya magharibi ambayo huwa na balozi mjini Pyongyang , kama vile Ujerumani, wanaona kuna thamani kubwa ya kuweka mawasiliano yao na taifa hilo wazi yakiamini kwamba uhusiano wa kidiplomasia ndio suluhu bora ya kutatua tatizo la Korea.

Pia yanaweza kutoa huduma, kwa mfano, ni ubalozi wa Sweden ambao ulipewa ruhusa ya kumuona mwanafunzi wa Marekani Otto Warmbier, ambaye alikuwa amekamatwa mjini Pyonyang 2016 na kufariki muda mfupi aliporudishwa nchini Marekani

Maelezo ya picha,

Rais wa Marekani Donald Trump

Balozi wa zamani wa Uingereza mjini Pyonyang alidai kwamba kuna umuhimu mkubwa kuwa na ubalozi nchini Korea Kaskazini kwa sababu hakuna gharama nyingi na utakuwa katika hali nzuri ya kuchukua hatua kama jicho la jamii ya kimataifa mbali na kuwa masikio wakati wa hali mbaya.

Waziri wa maswala ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson amedai kwamba Marekani iko tayari kuzungumza na Korea Kaskazini iwapo itarudi katika meza ya mazungumzo.

Taasisi ya Lowy kuhusu uhusiano wa Kidiplomasia inaonyesha kwamba ni mataifa machache ambayo uhusiano wao unazidi kudidimia.

Ni mataifa manne kati ya yale 43 mwanachama wa OECD na mataifa ya G20 ambayo yamepunguza uhusano wao wa kidiplomasia katika kipindi cha miaka miwili licha ya bajeti za kukwamua uchumi wake tangu mgogoro wa kifedha.

Mataifa 20 yaliongeza uhusiano wao wa kidiplomasia ikiwemo, Hungary, Uturuki na Australia miongoni mwao.

Lengo la balozi kuwa kitengo muhimu cha kidiplomasia linaonekana kufaulu na kuendelezwa.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa taifa ambalo limetengwa zaidi duniani.

Huku ikiwa kuna uhusiano ,hata usiothabiti kati ya Pyonyang na ulimwengu, chaguo la kidiplomasia na Korea Kaskazini halijatumika na kumalizwa.