Mswada wa kupunguza kodi Marekani wajadiliwa na bunge la Seneti

Wabunge wa Republican wanasema mswada huo ni faida kwa wengi
Maelezo ya picha,

Wabunge wa Republican wanasema mswada huo ni faida kwa wengi

Maseneta wa Marekani wanajadili mswada ambao unaweza kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa Kodi ambao umekuwepo kwa zaidi ya miongo mitatu nchini humo.

Wabunge wa bunge la wawakilishi awali walipiga kura upande wa mabadiliko makubwa ambayo ikiwa yatapitishwa itakuwa ni mafanikio ya kwanza makubwa ya Rais Trump katika utawala wake.

Kura za Seneti zinategemewa kupigwa saa chache zijazo.

Maelezo ya picha,

Wabunge wa Democratic wanasema mpango huo utayanufaisha makampuni makubwa pekee

Hata hivyo, maamuzi ya mwisho yatalazimika kusubiri hapo baadae ambapo mswada utakuwa umerejeshwa bungeni kwa lengo la kukamilisha utaratibu ,kabla ya Rais Trump kutia saini ili kuwa sheria kamili.

Msemaji wa Republican Paul Ryan amesema iwapo sheria hiyo itapita, itawanufaisha raia wengi hususan wa kipato cha chini.

Kwa upande wa wabunge wa Democratic wanasema maamuzi hayo yanawanufaisha makampuni makubwa na matajiri.

Mswada huu ukoje?

Unatafsiriwa na Rais Trump kama zawadi ya sikukuu za Christmass na mwaka mpya kwa wananchi wote, huku mbunge wa Democratic Barbara Lee akisema ni sawa na kuzipiga kofi kali la usoni familia za kipato cha chini na kati.

Inatarajiwa kukata kodi kwa makampuni kutoka asilimia 35 mpaka 21.

Inapunguza kodi kwa mashirika makubwa sambamba na kima cha kati kwa makampuni mengine.

Inatarajiwa pia kupunguza kodi kwa watu binafsi.

Maelezo ya picha,

Rais Trump amekuwa akikumbana na upinzani mkali kutoka Democratic

Nini kinatarajiwa?

Mpaka sasa mjadala mkali unaendelea, kila pande ikibishana kwa hoja na baadae kura zitapigwa.

Makamu Rais wa Marekani Mike Pence ameahirisha ziara yake kwa nchi za Mashariki ya kati ili kuwepo kama atahitajika.

Siku ya jumatatu, wabunge pakee wa Republican waliokuwa wakiupinga mswada huo Susan Collins na Mike Lee walikubali kuupigia kura ikimaanisha kuongeza uwezekano zaidi.

Iwapo mswada huu utapitishwa, utakuwa ni ushindi mkubwa kwa Trump tokea aingie madarakani.

Maelezo ya picha,

Wabunge wa Republican wanatumai kuupitisha mswada huo kabla ya sikukuu za mwisho wa mwaka

Kwanini mswada huu ni muhimu?

Licha ya kuwa iwapo mswada huu utapitishwa utakua na matokeo makubwa kwa wananchi wa Marekani, chama cha Republican kinataka kuonyesha kuwa kina nguvu baada ya kushindwa katika mswada wa awali wa bima ya afya maarufu kama Obamacare.