'Nilibakwa na watu watatu' : Mama anaeleza masaibu yake wakati wa uchaguzi Kenya

Image caption 'Walikuja nyumbani kwangu wakati nilipokuwa nimelala.' - Elizabeth Adera

Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch hivi karibuni lilitoa ripoti inayosema kwamba maafisa wa polisi nchini walishiriki katika vitendo vya ubakaji wakati wa uchaguzi wa mwezi wa Agosti.

Mwana mama Elizabeth Adera anayedai kubakwa na polisi akiwa nyumbani kwake, mjini Kisumu ameieleza BBC yale yaliyomtokea hapa chini:

Mmoja akanisukuma na mwingine akinishika na huku akinirarua suruali. Wakaniingilia.

Walianza kuambiana "Maliza nataka niingie!"

Nilibakwa na watu watatu.

Nikaanza kupiga kelele kwa uchungu niliokuwa nausikia.

Nikawaambia kuwa "jamani, mimi ni mjane, na hata kama mnanifanya hivi, tayari, mimi ni mtu ninayeishi na virusi. Mimi nina ukimwi, mnihurumie."

Hapo ndipo wakaniacha, wakanisukuma na nikajigonga vibaya

Wakachukua maboksi mawili ya samaki ambao nilikuwa nimewaanda kwaajili ya kuuza kesho yake, pamoja na fedha dola 80.

'Naogopa Polisi'

Cha kushangaza ni kwamba hawakushtuka nilipowaambia kwamba nina virusi.

Tayari sasa ,wamepata ukimwi, kwa sababu hawakutumia kinga yoyote.

Naona lengo lao lilikuwa kuniumuza kabisa ili nibaki na kumbukumbu hiyo ambayo sitaisahua milele hadi kifo changu.

Sasa nawaogopa sana polisi, nikiwaona tu, nataka kukimbia.

Watoto wangu hadi leo wamebaki na huzuni na mimi bado nina maumivu.

Kwa bahati mbaya, watoto walikuwepo wakati polisi hao waliponitendea ukatili huo. Mjukuu wangu,ni msichana wa kidato cha pili pamoja na kijana wangu walisikia yote walionitenda na walivyokuwa wananiambia.

Walikuja nyumbani kwangu wakati nilipokuwa nimelala. ikujua kwamba wangeweza kunifanyia matendo kama hayo. Sijui sababu ya hao watu kutudhulumu. Niliwaambia mimi ni mjane ninaishi tu na watoto wangu. Mimi sijawahi kutoka nje, kurusha mawe.

Haki miliki ya picha MARCO LONGARI/AFP
Image caption Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema kuwa vikosi vya usalama nchini Kenya vilitekeleza vitendo vya ukatili wa kingono wakati na baada ya uchaguzi wa urais wa mwezi Agosti.

'Roho ya Unyama'

Tangu siku hiyo, maisha yangu yamekuwa magumu sana. Kwa miezi miwili baada ya tukio hilo,nimebaki nyumbani huku nikiwa siwezi kutembea. Walinigonga sana na waliniumiza mgongo. Hao watu hawakuwa na roho ya ubinadamu, walikuwa na roho ya unyama.

Ningeomba serikali ya Kenya wawafundishe vikosi vya polisi namna ya kushughulika na raia kwa ubinadamu. Mtu akifanya makosa, afadhali akamatwe na kufunguliwe mashtaka.