Korea Kaskazini: Marekani inapanga kutekeleza ''uhalifu''

Marekani imemuonya rais Kim Jong Un wa Korea Kaskazini kusitisha majaribio yake ya silaha Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marekani imemuonya rais Kim Jong Un wa Korea Kaskazini kusitisha majaribio yake ya silaha

Katika siku ambayo baraza la usalama la Umoja wa mataifa linapiga kura kuidhinisha vikwazo vikali zaidi dhidi ya Korea kaskazini, kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong-un, amesema taifa lake linawakilisha tishio kubwa la nyuklia kwa Marekani.

Katika hotuba iliyoripotiwa na shirika la utangazaji habari nchini (KCNA) Kim amesema kuendelezwa kwa haraka kwa mpango wa nchi yake wa nyuklia kunashinikiza ushawishi muhimu katika siasa za kimataifa.

Azimio la hivi karibuni la baraza hilo la usalama katika Umoja wa mataifa linalenga kupiga marufuku usafirishaji wa bidhaa zote za mafuta kwenda Pyongyang na kuitisha kurudishwa kwa raia wa Korea Kaskazini wanaofanya kazi katika nchi za nje katika muda wa mwaka.

Korea Kaskazini imetaja nakala za kiusalama za Marekani zinazosisitiza kuhusu utumizi wa mabavu dhidi ya Pyongnyang kuwa za kihalifu, vyombo vya habari vya taifa hilo zimesema.

Wizara ya maswala ya kigeni ilimlaumu rais wa Marekani Donald Trump kwa kutaka kukandamiza ulimwengu kupitia sera yake mpya ya usalama.

Image caption Rais Trump amesema kuwa Marekani itatumia nguvu dhidi ya Pyongyang

Siku ya Jumatatu rais Trump alisema kuwa Washington lazima ikabiliane na changamoto inayoletwa na mpango wa kutengeza silaha wa Pyongyang.

Msemaji wa wizara ya maswala ya kigeni nchini Korea Kaskazini amesema kuwa mpango mpya wa Marekani kuhusu usalama hauna lolote bali mpango wa kutaka kutumia nguvu kulingana na chombo cha habari cha kitaifa KCNA.

Ameilaumu Marekani kwa kutaka kujaribu kuvuruga taifa hilo na kugeuza rasi yote ya Korea kuwa eneo litakalotawaliwa na Marekani.

Siku ya Jumatatu rais Trump alielezea kuhusu mpango huo mpya akiikosoa Korea Kaskazini kwa kufanya majaribio ya silaha za kinyuklia licha ya shutuma kutoka Marekani na Umoja wa Mataifa.

Mwezi uliopita, rais wa Marekani pia aliliweka taifa la Korea Kaskazini miongoni mwa mataifa yanayofadhili ugaidi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii