Jenerali wa jeshi aliyemng'oa Mugabe sasa ni naibu wa Zanu-PF

Constantino Chiwenga, alistaafu hivi karibuni kama mkuu wa jeshi, na kuzusha tetesi, kwamba atapewa wadhifa wa kisiasa.
Maelezo ya picha,

Constantino Chiwenga, alistaafu hivi karibuni kama mkuu wa jeshi, na kuzusha tetesi, kwamba atapewa wadhifa wa kisiasa.

Jenerali wa Zimbabwe, aliyeongoza mapinduzi yaliyopelekea Robert Mugabe kuondoshwa madarakani, ameteuliwa kuwa naibu kiongozi wa chama tawala cha ZANU-PF.

Uteuzi huo ulifanywa na rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Constantino Chiwenga, alistaafu hivi karibuni kama mkuu wa jeshi, na kuzusha tetesi, kwamba atapewa wadhifa wa kisiasa.

Uteuzi huo, unaonekana kama hatua ya kuelekea kutajwa kuwa makamo rais.Makamu mwengine wa Zanu PF ni Kembo Mohadi ambaye alikuwa waziri usalama chini ya Robert Mugabe.

Hatua hiyo ya uchukuaji mamlaka mnamo tarehe 15 Novemba inajiri siku kadhaa baada ya Mnangagwa ,wakati huo akiwa makamu rais alifutwa kazi na Mugabe na kuondoka nchini humo.

Maelezo ya picha,

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Hatua hiyo ilionekana kama jaribio la kumuweka mke wa Mugabe kuwa mrithi wake badala ya Mnangagwa.

Lakini bwana Mnangagwa alikuwa na uhusiano mkubwa na Jeshi na kufuatia kuingilia kati kwa jeshi aliteuliwa kuwa rais na kuapishwa tarehe 24 mwezi Novemba.

Kama Mnangagwa , bwana Chiwenga alikuwa mwandani wa Mugabe akiwa kiungo muhimu katika kuchukua mashamba ya watu weupe mbali na kuwasaka maafisa wa upinzani baada ya uchaguzi 2008.

Lakini anasemekana kuwa tayari kuokoa uchumi wa Zimbabwe ambao anaamini uko hali mbaya inayoweza kutishia usalama wa kitaifa.

Tayari rais Mnangagwa amewateuwa wanajeshi wawili wa zamani kuwa mawaziri.

Mnamo Novemba 30, aliyekuwa jenerali Sibusiso Moyo ambaye alikuwa kiungo muhimu katika unyakuzi huo wa mamlaka aliteuliwa kuwa waziri wa maswala ya kigeni huku mkuu wa jeshi la angani Perence Phiri akipewa wadhfa wa kiilimo na ardhi.