Mkusanyiko wa habari za Tanzania 2017

Image caption Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Sababu ya CCM kuendelea kuongoza Tanzania

Shughuli ya kusukwa upya kwa safu ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania itahitimishwa wiki hii katika mkutano mkuu unaofanyika mjini Dodoma, katikati mwa nchi hiyo.

Huu ni uchaguzi wa kwanza tangu Rais John Magufuli aliporithi uenyekiti kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.

CCM inaendeleza mikakati ya kurejesha hadhi yake baada ya ushindi uchaguzi wa mwaka 2015.

Licha ya kushinda urais kwa taabu, wapinzani chini ya mwamvuli wa UKAWA walipata karibu theluthi moja ya viti vyote vya ubunge na kudhibiti halmashauri katika miji muhimu ikiwemo Dar es Salaam, hii ikiwa ni rekodi mpya.

Miaka miwili ndani ya utawala wa Rais Magufuli, upepo unaonekana kugeuka.

Tanzania yaongeza maradufu panya wanaotambua TB

Tanzania inaongeza maradufu idadi ya panya buku wanaotumika kuutambua ugonjwa wa kifua kikuua.

Panya hao hupewa mafunzo na wana uwezo wa kunusa kamasi za binaadamu na kutambua kwa haraka ugonjwa wa TB.

Wana uwezo wa kutambua sampuli mia moja kwa muda usiozidi dakika 20.

Tofuati na binaadamu - wataalamu wa maabara wanaotumia siku nne kuchunguza idadi hiyo ya sampuli.

Tanzania sasa itawatumia panya hao katika kliniki zipatazo 60 kote nchini.

Tanzania yajitenga na Trump kuhusu Jerusalem

Tanzania imesema haikubaliani na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania kupitia taarifa imesema nchi hiyo inaunga mkono makubaliano ya kimataifa ambayo yanatambua haki ya watu wa Palestina kumiliki Mashariki mwa Jerusalem kama ilivyokuwa kwenye mpaka wa kabla ya mwaka 1967.

"Tanzania inaunga mkono msimamo wa Umoja wa Mataifa wa suluhu ya mataifa mawili ambayo unatoa nafasi ya Israel na Palestina kuwepo kwa pamoja zikiwa na mipaka salama," taarifa hiyo iliyotuwa saini na Waziri Augustine Mahiga imesema.

Bw Trump kando na kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, alisema nchi hiyo pia itahamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv.

Bw Mahiga amesema ubalozi wa Tanzania utaendelea kuwepo mjini Tel Aviv.

Msimamo wa Tanzania unaenda sambamba na msimamo wa mataifa mengi ya Afrika pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Walinda amani wa Tanzania wauawa DR Congo

Umoja wa Mataifa umethibitisha kwamba walinda amani 14 wa muungano huo waliuawa na wengine 53 kujeruhiwa baada ya kambi yao kuvamiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kati ya waliouawa, angalau wanajeshi 12 walitoka Tanzania.

Katibu mkuu huyo ameshutumu vikali shambulio hilo na kusema ni sawa na uhalifu wa kivita.

Ameitaka DR Congo kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na kusema kwamba waliohusika wanafaa kuwajibishwa.

Wanajeshi zaidi wametumwa eneo hilo na kamanda wa kikosi cha kulinda amani anaelekeza shughuli ya kuwaondoa majeruhi.

Bw Guterres amesema shambulio hilo ndilo mbaya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.

Huwezi kusikiliza tena
Tundu Lissu: Kushambuliwa kwangu kulichochewa na siasa Tanzania

Dhuluma wanazopitia uarabuni wafanyakazi wa nyumbani kutoka Tanzania

Wafanyakazi wa kike wa nyumbanni kutoka nchin Tanzania walio nchini Oman na milki ya nchi za kiarabu UAE, wanadhulumiwa kimwili na kingono, wakiwa wanafanya kazi masaa mengi na wakilipwa mishahara midogo, kwa mujibu wa shirika la kitetea haki za binadamu, Human Rights Watch (HRW).

Kwenye ripoti iliyotelewa leo, HRW ilisema kuwa kuna maelfu ya wafanyakazi wa nyumbani kutoka Tanzania wako nchini Oman na UAE.

Watafiti wake waliwahoji 50 kati yao na kugundua kuwa karibu wote walipokonywa pasipoti zao walipowasili na kulazimiswa kufanya kazi hadi masaa 21 kwa siku bila kupumzika.

Kwa nini Tanzania ikawapiga mnada ng’ombe kutoka Kenya

Serikali ya Tanzania imetetea hatua yake ya kuwakamata na kuwapiga mnada mifugo pamoja na kuteketezwa kwa vifaranga kutoka nchi jirani ya Kenya.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kupitia taarifa kwamba Tanzania ilifuata utaratibu uliopo kisheria na kwamba mataifa hayo mawili yamekuwa yakiwasiliana.

Waziri wa mambo ya nje nchini Kenya Amina Mohamed ameilalamikia serikali ya Tanzania kufuatia hatua ya taifa hilo.

''Tulidhani kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yangetatua mzozo huu, lakini tulishindwa kuafikia makubaliano. Ni wakati huo ambapo tuliamua kuzungumza na balozi wetu nchini humo kuwasilisha barua ya kupinga hatua ya kuwapiga mnada mifugo hao''.

''Historia ambayo tumekuwa nayo na Watanzania ni nzuri sana na kila kunapotokea tatizo tumekuwa tukitatua.Ni kwa sababu hiyo ambapo imekuwa hatua ya kushangaza miongoni mwa wafugaji wa Kenya'', waziri huyo alizungumza katika mkutano na vyombo vya habari.

Magufuli: Tanzania sio shamba la mifugo wa taifa jirani

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwakamata mifugo watakaoingia nchini humo kutoka taifa jirani.

Akizungumza katika mkoa wa Kagera ambako ameanza ziara yake ya kikazi Magufuli amesema kwamba Tanzani sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani na kwamba ataichukulia mifugo hatua kali za kisheria mifugo yoyote.

Vilevile ameitaka nchi Jirani kuchukua hatua kama hiyo iwapo mifugo ya Tanzania itaingia nchini humo kinyume na sheria.

Serikali ya Tanzania yalifungia gazeti la Tanzania Daima kwa siku 90

Serikali ya Tanzania kupitia idara ya habari maelezo imelifungia Gazeti la Tanzania Daima ambalo ni gazeti la kila siku,kwa muda wa kwa siku 90 .

Tamko hilo pia limepiga marufuku toleo la mitandaoni la gazeti hilo. Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji mkuu wa serikali Tanzania Dr, Hassan Abbas, amesema gazeti hilo limefungiwa kutokana na ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya habari ikiwemo kuchapisha habari za uongo na za kichochezi ambazo zinaweza kuzusha hofu miongoni mwa jamii.

Miongoni mwa habari zilizosababisha kufungwa kwa gazeti la Tanzania Daima , ni ile iliyokuwa na makosa ya kihariri kwenye toleo namba 4706 la Oktoba 22, 2017 ambalo liliandika kuwa 'ASILIMIA 67 YA WATANZANIA WANATUMIA ARVS' dawa za kufubaza makali ya ugonjwa wa ukimwi, habari nyingine katika toleo hilo ilieleza kuwa "MAKINIKIA PASUA KICHWA". Idara hiyo imedai kuwa gazeti hilo limetoa habari yenye uongo wenye nia ya kuleta dharau dhidi ya hatua ya serikali na makubaliano yaliyofikiwa baina yake na kampuni ya Barrick Gold Corporation.

Barrick Gold kuilipa Tanzania dola milioni 300 za kimarekani

Kampuni ya inayomiliki migodi ya madini nchini Tanzania, Barrick Gold imekubali kuilipa Serikali ya Tanzania hisa ya asilimia 16 na mgawo wa asilimia hamsini ya mapato ya mauzo ya dhahabu kutoka migodi 3 inayoimiliki.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria mpya za madini ya Tanzania baada ya kampuni hiyo kukubali kuwa na mazungumzo na Serikali ya Tanzania .

Vilevile kampuni hiyo imekubali kutoa Dola za Kimarekani milioni 300 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara ya kampuni hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo,Prof. Thornton amesema Barrick Gold Corporation watazingatia makubaliano haya na wanaamini kuwa yamefungua ukurasa muhimu utakaowezesha kufanya biashara kisasa.

Huwezi kusikiliza tena
Je wajua mende ni lishe bora?

Tanzania yawatimua mawakili 3 wa Afrika Kusini

Tanzania imewafurusha mawakili watatu wa Afrika Kusini waliokamatwa wiki hii wakituhumiwa kwa kukuza mapenzi ya jinsia moja.

Walikuwa miongoni mwa watu 13 waliokamatwa katika hoteli moja mjini Dar es Salaam .

Waandalizi wa mkutano huo wanasema kwamba mkutano huo ulikuwa umeitishwa kujadili iwapo wakabiliane na uamuzi wa serikali ya Tanzania kuzuia utoaji wa baadhi ya huduma za afya.

Rais Magufuli: Mshahara wangu ni shilingi milioni 9 za Tanzania

Rais wa Tanzania John Magufuli amefichua kuwa anapokea mshahara wa kila mwezi wa shilingi milioni 9 za Tanzania.

Hii ni robo ya mshahara ambao mtangulizi wake Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa akipokea iwapo takwimu zilizonakiliwa na Afrika Review miaka mitatu iliopita ni za kweli.

Rais Magufuli alifichua hayo katika taarifa ya moja kwa moja katika runinga mapema Jumanne katika hotuba kwa muungano wa serikali za mitaani wakati ambapo alikuwa akikisisitiza kuhusu umuhimu kwa kukabiliana na rushwa.

''Baadhi ya wanachama wa bodi za mashirika ya uma walikuwa wakisafiri hadi Dubai kufanya mikutano yao huko ili wajilipe marupuru mengi.Hivi sasa hawataki kile serikali yangu inachofanya''.

Pacha walioshikamana wajiunga na chuo kikuu Tanzania

Ni ndoto iliozaa matunda kwa pacha walioshikana Maria na Consalata nchini Tanzania baada ya kuanza masomo yao katika chuo kikuu ili kujifunza kuwa walimu.

Kulingana na gazeti la The Citizen, waliwashukuru walimu wao wapya kwa mapokezi mema waliopata mbali na mazingira mazuri ya kusoma waliopata yalioandaliwa na chuo kikuu cha Ruaha Catholic University.

Waliwasili katika chuo hicho mbele ya wanafunzi wengine ili kuweza kujiandaa na mazingira yaliyopo.

Walianza masomo yao ya Kompyuta siku ya Jumatano .Waliwashukuru Wamishenari wa Consalata kwamba wamefikia kiwango hicho cha maisha yao.

Wamishenari hao waliwalea na kuwashawishi kuendelea na masomo.

Huwezi kusikiliza tena
Tanzania: Adui wa mwanamke kiuchumi ni mwanamume?

Tanzania yahusishwa na Korea Kaskazini

Tanzania imesema imeshtushwa baada ya kuorodheshwa miongoni mwa nchi ambazo zimechunguzwa na Umoja wa Mataifa na kuhusishwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na Korea Kaskazini.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, waziri wa mambo ya nje Dkt. Augustine Mahiga, amesema licha ya uhusiano uliokuwepo awali, lakini tangu mnamo mwaka 2014, Tanzania imepunguza kabisa uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia na nchi hiyo.

"Hatuna ugomvi na Korea Kaskazini,lakini kitendo chao cha kutengeneza masilaha ya kuangamiza sio mazuri kwa heshima na usalama duniani.Ndiyo maana tukaanza kuchukua hizo hatua za kupunguza mahusiano." amesema Dr Mahiga kwa waandishi wa habari leo.

Waziri Mahiga ameongeza kusema kuwa, uhusiano huo wa kibiashara ulikuwepo kabla ya vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni na Baraza la Umoja wa Mataifa.

Serikali yafuta leseni za Magazeti Tanzania

Magazeti na machapisho yote ya habari nchini Tanzania yatasajiliwa upya kuanzia tarehe 23 mwezi Agosti hadi Octoba 15 ,2017 ikiwa ni utekelezaji wa kifungu cha tano (e) cha Sheria ya Huduma za habari 2016.

Agizo hilo lilotolewa na Idara ya Habari Maelezo kupitia Mkurugenzi wake ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali Dr. Hassan Abbas, linayahusu magazeti na machapisho yote ya habari ambayo yalipatiwa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo tayari imefutwa.

Utoaji huo wa leseni pia ni kwa mujibu wa Kanuni ya 7 ya Kanuni za Sheria ya huduma za habari za mwaka 2017 zilizochapishwa kwa mujibu wa tangazo la serikali Na 18 la Februari 3, 2017

Acacia ''yakataa'' kuilipa Tanzania $180b

Serikali ya Tanzania imesema kuwa kampuni ya kuchimba dhahabu yenye makao yake nchini Uingereza Acacia inadaiwa na walipa kodi dola bilioni 180 ,kama malipo ya adhabu na riba, kulingana na taarifa ya kampuni hiyo.

Takwimu hiyo ni kulingana na ufichuzi uliofanywa na tume mbili za rais kuhusu sekta ya uchimbaji madini.

Kulingana na mwandishi wa BBC Sammy Awamy deni hilo linalodaiwa Acacia linasimamia mapato yaliopatikana ambayo hayakutajwa kutoka kwa migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi katika kipindi cha mwaka 2000 na 2017.

Gazeti jengine lafungiwa Tanzania

Gazeti la Raia Mwema ambalo ni gazeti la kila wiki, limefungiwa na serikali ya Tanzania kwa siku 90 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo.

Idara hiyo imeeleza sababu za kusitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo kuwa ni kutokana na kuchapishwa kwa toleo la tarehe 27 mwezi Septemba hadi 3 Oktoba 2017, lenye kichwa cha habari inayosomeka, "URAIS UTAMSHINDA JOHN MAGUFULI."

Idara hio imedai kuwa gazeti hilo limetoa nukuu zisizo za ukweli kuhusu Rais John Magufuli, japo imekubali kuwa ni haki ya gazeti hilo kutoa maoni. Kusitishwa kwa gazeti hilo ni pamoja na toleo ya mtandaoni.

Washindi watuzwa kombe la Charity ''Sheild'' kimakosa Tanzania

Makosa ya herufi yanaweza kuwa ndoto mbaya kwa mwandishi yeyote yule.

Hatahivyo makosa hufanyika na binadamu yeyote yule na anapotambua makosa hayo yeye husahihisha.

Lakini sio kama makosa ya herufi katika kombe kubwa la soka.

Siku ya Jumatano usiku klabu ya Simba iliwalaza wapinzani wao wa jadi Yanga kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya kombe la kufungua msimu la Community Shield.

Tanzania na Kenya kuondoleana vikwazo vya kibiashara

Mataifa ya Tanzania na Kenya yalifanikiwa kuandaa mkutano ambao utapelekea kuondolewa kwa marufuku ya bidhaa zinazoingia katika mataifa hayo mawili kutoka pande zote mbili.

Waziri wa maswala ya kigeni na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga alitangaza uamuzi huo jijini Nairobi kufuatia majadiliano kati ya rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Na kufuatia hatua hiyo Kenya itaondoa marufuku ya Unga wa ngano na Gesi inayoingia nchini humo kutoka Tanzania huku Tanzania nayo ikiondoa marufuku ya sigara na maziwa kutoka Kenya.

Simba apatikana akimnyonyesha mwana wa Chui Tanzania

Mwana wa chui hawezi kubadili madoa doa katika ngozi yake lakini simba huyo hajali hilo.

Picha hizi ni za kwanza kuchukuliwa simba akimnyonyesha mwana wa chui kutoka jamii nyengine ya wanayama, kisa kisicho cha kawaida.

Wawili hao walionekana na Joop Van Der Linde mgeni katika katika eneo la Ndutu safari Lodge nchini Tanzania katika eneo la uhifadhi la wanyma pori la Ngorongoro.

Usher Raymond azuru mbuga ya Serengeti Tanzania

Msanii wa Marekani Usher Raymond yuko ziarani nchini Tanzania akitembelea eneo la uhifadhi wa wanyama pori la Serengti National Park.

Bwana Raymond alichapisha baadhi ya picha akiwa na familia yake katika akaunti yake ya Twitter.

Alielezea hali ilivyo katika eneo hilo kama ya kufurahisha .

Ripoti za Usher Raymond kuzuru Tanzania zilisambaa kwa haraka nchini humo.

Tundu Lissu apigwa risasi Tanzania

Mwanasiasa huyo amekimbizwa hospitali ya mkoa wa Dodoma na kupokea huduma ya kwanza na taarifa zinasema kuna mipango ya kumsafirisha hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

Rais wa Tanzania John Magufuli kupitia kwenye Twitter amesema amesikitishwa sana na kushambuliwa kwa mbunge huyo.

Ameandika: "Nimepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi Mh. Tundu Lissu, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka. Aidha, vyombo vya dola viwasake wale wote waliohusika na tukio hili la kinyama na kuwafikisha ktk mikono ya sheria."

Mambo muhimu kuhusu sakata ya madini Tanzania

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki hii alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof John L Thornton.

Taarifa kutoka ikulu baada ya mkutano huo ilisema walikubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli nchini Tanzania.

Baada ya Mazungumzo hayo Prof Thornton aidha alinukuliwa akisema kuwa kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.

Mada zinazohusiana