Mahakama: Bunge lilishindwa kumuwajibisha rais Jacob Zuma

Rais Jacob Zuma alidaiwa kutumia mamilioni ya dola kurekebisha na kupamba jumba lake la Nkandla. Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Jacob Zuma alidaiwa kutumia mamilioni ya dola kurekebisha na kupamba jumba lake la Nkandla.

Mahakama ya kilele ya Afrika kusini imesema kwamba bunge la nchi hiyo halikutimiza wajibu wake ipasavyo kwa kushindwa kumuwajibisha Rais Jacob Zuma kuhusu madai ya ufujaji wa mamilioni ya dola zilizotumika kurekebisha na kupamba jumba lake la Nkandla.

Ingawa mahakama hiyo ya upeo zaidi inakiri kwamba ni kweli bunge la Afrika kusini lilifanya kikao cha maswali na majibu kuhusu kashfa hiyo na hata kupigia kura mswaada wa kutokuwa na imani lakini linasema hatua hizo zote hazitoshi kumuajibisha Rais Zuma.

Akisoma uamuzi wa mahakama hiyo Jaji Chris Jafta amesema bunge ni sharti wakati wote litimize wajibu wake wa kumuwajibisha rais bila ya kuchelewa.

Mahakama hiyo pia imeliamuru bunge hilo la Afrika Kusini kulipa gharama za kesi hiyo.

Hata hivyo Jaji mkuu Mogoeng Mogoeng amehitilafiana na uamuzi huo akisema mahakama hiyo imepita mipaka yake na kuingilia mihimili mengine ya utawala.

Lakini Chama tawala cha Africa National Congress kimetoa taarifa kikisema kwamba kitatazama kwa makini uamuzi huo wa mahakama ya kilele na kujadili kikamilifu athari za uamuzi huyo katika kikao kamili cha baraza kuu la chama tawala katika muda wa majuma mawili yajayo.

Kesi hii imetokana na kima cha dola milioni 16 ,fedha za serikali zilizotumiwa na Rais Zuma mwaka 2014 katika kurekebisha na kupamba jumba lake la kibinafsi la Nkandla.

Awali alikuwa ameamriwa kurudisha kiasi fulani cha pesa hizo lakini hakufanya hivyo.

Mada zinazohusiana