Vitisho vya kuyafuta mashirika ya kidini vyazua hisia Tanzania

Zachary Kakobe Haki miliki ya picha facebook/Zachary Kakobe
Image caption Zachary Kakobe

Vitisho vya afisa wa ngazi ya juu nchini Tanzania vya kutaka kufutilia mbali leseni za mashirika ya kidini ambayo viongozi wake wanazungumza siasa vimezua hisia kali nchini humo.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania wanaharakati wa haki za kibinaadamu, wanasiasa kutoka chama tawala na vile vya upinzani, wachanganuzi wa kisiasa na viongozii wa dini walishutumu vitisho hivyo vilivyotolewa na katibu wa kudumu wa maswala ndani Projest Rwegasira kama yasiofaa, wakidai ni njia nyengine ya kutaka kuwanyamazisha wakosiaji wa serikali.

Onesmo Olengurumwa kutoka Shirika la haki za kibinaadamu la Tanzania Human Rights Defenders Coalition , alivishutumu vitisho hivyo akisema havina uhalali wowote.

''Kuna tofauti kubwa kati ya kushiriki katika siasa na kutoa maoni ya kisiasa'', alisema.

Olengurumwa mbaye ni wakili alisema kuwa kushiriki katika siasa kunashirikisha uchaguzi na kufanya kampeni za kugombea wadhfa wa kisiasa.

Naye Profesa Bakari Mohammed ,ambaye ni muhadhiri katika chuo kikuu cha Dar es Salaam alisema: Kile kinachoshangaza ni kwamba vitisho hivi na onyo hutolewa wakati serikali inapokosolewa na sio wakati viongozi hao wa dini wanapoipongeza.

Katika taarifa iliotolewa siku ya Alhamisi kwa mujibu wa gazeti la The Citizen, katibu huyo wa kudumu aliambia viongozi wa dini kutotumia mimbari zao kuzungumza siasa.

Alitishia kuyapokonya leseni mashirika ambayo yanaenda kinyume na sheria ya kijamii ambayo inawataka kuzingatia malengo yao pekee.

Onyo lake linajiri siku chache baada ya viongozi wa dini kutumia hotuba zao za siku kuu ya Krisimasi kuonyesha wasiwasi wao kuhusu hali ya uhuru wa kujieleza.

KIongozi wa dini Zachary Kakobe, alitumia hotuba ya Krisimasi kusema kuwa taifa 'linarudi kuwa taifa la chama kimoja'.

''Hakuna shirika lolote la kidini ambalo liliwasilisha katiba yake kwa msajili ambayo inahusisha maono ya kisiasa'', alisema bwana Rwegasira.

Kulingana na gazeti hilo, Dkt Hellen Kijo-Bisimba ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa shirika la haki za kibinaadamu la Human Rights Center LHRC , alisema kuwa viongozi wa kidini wana haki sawa za uhuru wa kujieleza kama ilivyo katika katiba.

''Kinachotushangaza ni kwamba vitisho hivi huwaendea wale wanaokosoa serikali na sio wale wanaoipongeza'', alisema Dr Kijo-Bisimba

Mwanaharakati huyo amevitaja vitisho hivyo kuwa muendelezo wa vitisho dhidi ya watu na makundi yanayoonekana kupinga serikali.

Mada zinazohusiana