Marekani yaipuuzilia mbali Iran kwa lawama kuhusu maandamano na kusema ni 'upuuzi'

Iranian students run for cover from tear gas at the University of Tehran during a demonstration Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kulitokea maandamano Chuo Kikuu cha Tehran Jumamosi

Marekani imepuuzilia mbali tuhuma za Iran kwamba maadui zake ndio wanaochochea wimbi la maandamano ambalo limekumba taifa hilo siku za karibuni.

Marekani imesema huo ni "upuzi mtupu".

Kiongoni mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema maadui wa Iran ndio wanaochangia maandamano hayo Jumanne, alipozungumza kwa mara ya kwanza kuhusu ghasia hizo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley hata hivyo alisema maandamano hayo yalikuwa ya "kuchipuka ghafla" na kuongeza kwamba Marekani inapanga kuitisha mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali taifa hilo la Ghuba ya Uajemi.

Maandamano hayo yalizuka Alhamisi na kufikia sasa watu 22 wameuawa.

Chanzo cha maandamano hayo yaliyoanzia katika jiji la Mashhad kilikuwa kupanda kwa bei za bidhaa pamoja na ufisadi.

Lakini baadaye yaligeuka na kuwa maandamano ya kuipinga serikali.

Hayo yakijiri, Rais wa Iran Hassan Rouhani alizungumza na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron Jumanne.

Bw Macron aliomba kuwepo utulivu na wakati wa mazunguzo hayo iliafikiwa pia kwamba ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa iliyokuwa imepangiwa kufanyika wiki ijayo iahirishwe.

Nini chanzo cha mzozo wa sasa wa Marekani na Iran?

Kwenye taarifa katika tovuti yake rasmi, kiongozi wa kidini wa Iran alisema: "Siku za hivi karibuni, maadui wa Iran wametumia njia nyingi ikiwa ni pamoja na fedha, silaha, siasa na mashirika ya kijasusi kuzua taharuki katika Jamhuri hii ya Kiislamu."

Wachanganuzi wa mambo wanasema aliyekuwa akirejelewa katika kusema "maadui" ni Iran, Marekani na Saudi Arabia.

Bi Haley alisema madai hayo ya Iran ni ya kushangaza.

Aliongeza: "Watu wa Iran wanalilia uhuru, watu wote wapenda uhuru ni lazima wasimame nao na kuwaunga mkono katika juhudi zao."

Bi Haley alisema Marekani itaitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili maandamano hayo dhidi ya serikali ya Iran.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran walikabiliana na maafisa wa usalama wikendi

Mwandishi wa BBC Nada Tawfik aliyeko New York anasema baraza hilo huangazia mambo yanayotishia amani na usalama kimataifa na haijaeleweka iwapo kuna uungwaji mkono wa kutosha miongoni mwa wanachama wa muungano huo wa kufanyika kwa mkutano kama huo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandamanaji wamekuwa wakimshutumu Ayatollah Ali Khamenei
Haki miliki ya picha EPA
Image caption Hassan Rouhani amekuwa akitoa ujumbe mkali lakini pia kuonekana kuunga mkono mkono maridhiano

Bi Haley aliendelea: "Uhuru uliowekwa kwenye mwafaka wa Umoja wa Mataifa unatishiwa nchini Iran.

Makumi ya watu wameuawa. Mamia ya watu wamekamatwa.

"Iwapo historia ya udikteta Iran itategemewa, basi tunafaa kutarajia ukiukaji mkubwa siku zijazo."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gari lililoteketezwa Tuyserkan nchini Iran mnamo 31 Desemba

Msimamo wa Marekani kuhusu mzozo huo, ambao umehusisha pia Donald Trump kuandika ujumbe kwenye Twitter, umeshutumiwa sana na viongozi wa Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Bahram Ghasemi alisema Trump anafaa kuangazia "masuala ya ndani ya taifa lake, mfano kuuawa kwa makumi ya watu ... na kuwepo kwa mamilioni ya watu wasio na makao na wenye njaa."

Watu zaidi ya 450 wamekamatwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Tehran siku tatu zilizopita.

Maandamano kama haya yamewahi kutokea?

Maandamano ya sasa ndiyo ya kwanza makubwa zaidi tangu yaliyotokea wakati wa uchaguzi uliokuwa na utata 2009.

Maandamano makubwa ya wakati huo yaliandaliwa na mamilioni ya wafuasi wa upinzani dhidi ya Rais Mahmoud Ahmadinejad.

Watu 30 waliuawa na wengine maelfu kukamatwa wakati wa maandamano hayo yaliyokuwa makubwa zaidi Iran tangu kutokea kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii