Jenerali asema maadui wa Iran wameshindwa

Pro-government marcher in Ahvaz, 3 Jan Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mfuasi wa serikali akipeperusha bendera katika maandamano jiji la Ahvaz

Mkuu wa kikosi cha wanajeshi maalum walinzi wa rais na taifa nchini Iran maarufu kama Revolutionary Guards amesema "waliotaka kuhujumu serikali" wameshindwa nchini humo, akizungumzia maandamano ya kupinga serikali ambayo yamekumba taifa hilo kwa siku kadha.

Meja Jenerali Mohammad Ali Jafari alitoa tangazo hilo huku maelfu ya waungaji mkono wa serikali wakiandamana kupinga waandamanaji waliokuwa wanaipinga serikali.

Maandamano hayo yalianza Alhamisi katika mji wa Mashhad na kufikia sasa watu 21 wameuawa.

Chanzo cha maandamano hayo kilikuwa kupanda kwa bei za bidhaa pamoja na ufisadi.

Lakini baadaye yaligeuka na kuwa maandamano ya kuipinga serikali.

Watu zaidi ya 450 wamekamatwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Tehran siku tatu zilizopita.

Maandamano ya sasa ndiyo ya kwanza makubwa zaidi tangu yaliyotokea wakati wa uchaguzi uliokuwa na utata 2009.

Jenerali amesema nini?

Jen Jafari amesema: "Leo, tunaweza kusema ndio mwisho wa juhudi za kuhujumu serikali za 96," akirejelea mwaka wa sasa - 1396 - kwa kalenda ya Kiajemi.

Amesema "kujiandaa vyema kwa vikosi vya usalama na wananchi kuwa macho" kumesaidia kushindwa kwa "maadui" na kwamba Walinzi hao waliingilia kati tu kwa njia ndogo katika mikoa mitatu.

Ameongeza kuwa: "Kulikuwa na watu 1,500 wakikuwa wengi sana eneo moja na watu hao wa kuzua vurugu hawakuzidi 15,000 kote nchini."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jen Jafari amesema waandamanaji wa kupinga serikali hawakuzidi 15,000

Jenerali huyo amewalaumu wapinzani wa mapinduzi, watetezi wa utawala wa kifalme na mamluki ambao walikuwa "wametangazwa na [waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani] kuzua fujo, vurugu na utovu wa usalama Iran."

Amesema maadui hao walijaribu kusababisha tishio la kiutamaduni, kiuchumi na kiusalama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu wa Iran.

Amekariri tamko la kiongoni mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliyesema maadui wa Iran ndio wanaochangia maandamano hayo alipozungumza kwa mara ya kwanza kuhusu ghasia hizo Jumanne.

Wengi wanaamini alikuwa anazungumzia Marekani, Israel na Saudi Arabia.

Lakini Jenerali huyo pia amemlaumu "kiongozi wa zamani" kwa maandamano hayoakionekana kumzungumzia rais wa zamani Mahmoud Ahmadinejad ambaye amekuwa akikosoa viongozi wa serikali, hasa mkuu wa mahakama Sadegh Amoli Larijani wiki za karibuni.

Maandamano ya kuunga mkono serikali leo yamefanyika pia katika miji ya Kermanshah, Ilam na Gorgan.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa serikali katika mji wa Ahvaz

Marekani Jumanne ilipuuzilia mbali tuhuma za Iran kwamba maadui zake ndio wanaochochea wimbi la maandamano ambalo limekumba taifa hilo siku za karibuni.

Marekani ilisema huo ni "upuzi mtupu".

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley alisema maandamano hayo yalikuwa ya "kuchipuka ghafla" na kuongeza kwamba Marekani inapanga kuitisha mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali taifa hilo la Ghuba ya Uajemi.

Bi Haley aliendelea: "Uhuru uliowekwa kwenye mwafaka wa Umoja wa Mataifa unatishiwa nchini Iran.

Makumi ya watu wameuawa. Mamia ya watu wamekamatwa.

"Iwapo historia ya udikteta Iran itategemewa, basi tunafaa kutarajia ukiukaji mkubwa siku zijazo."

Maandamano kama haya yamewahi kutokea?

Maandamano ya sasa ndiyo ya kwanza makubwa zaidi tangu yaliyotokea wakati wa uchaguzi uliokuwa na utata 2009.

Maandamano makubwa ya wakati huo yaliandaliwa na mamilioni ya wafuasi wa upinzani dhidi ya Rais Mahmoud Ahmadinejad.

Watu 30 waliuawa na wengine maelfu kukamatwa wakati wa maandamano hayo yaliyokuwa makubwa zaidi Iran tangu kutokea kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii