Mlevi asafiri nchi tatu kwa kutumia teksi Ulaya mkesha wa Mwaka Mpya

A canal in Copenhagen lined with attractive multi-coloured buildings Haki miliki ya picha JONATHAN NACKSTRAND/AFP/Getty Images
Image caption Mwanamume huyo alikuwa akinywa pombe Copenhagen, mji mkuu wa Denmark

Mkazi mmoja wa mji wa Oslo anajutia aliyoyafanya akiwa amelewa mkesha wa Mwaka Mpya baada ya kugundua kwamba alikuwa anadaiwa $2,220 (£1,640) kwa kutumia teksi.

Mwanamume huyo wa miaka 40 hivi alikuwa amesafiri kupitia mataifa matatu, kuanzia Copenhagen nchini Denmark, akapitia Sweden, na kisha akafika Oslo nchini Norway.

Alipofika nyumbani, alikosa kumlipa nauli dereva wa teksi.

Dereva huyo alijipata amekwama baada ya betri ya gari lake yake kuisha chaji akiwa nje ya nyumba ya mwanamume huyo akisubiri atoke nje na pesa amlipe.

Aliamua kuwapigia polisi.

Kupitia Twitter, polisi wa Olso wanasema walimpata mwanamume huyo akiwa amelala fo fo fo kitandani na kumwamsha.

Alikubali kulipa pesa alizokuwa anadaiwa.

Mwanamume huyo hana historia ya kutekeleza uhalifu, kwa mujibu wa runinga ya taifa ya Norway ya NRK.

Safari hiyo ya kutoka Copenhagen hadi mtaa wa Abildso mjini Oslo ilikuwa ya umbali wa 600km (maili 372).

Huenda akafikiria kutumia ndege siku zijazo...

Na dereva wa teksi? Gari jingine lilifika kumsaidia..

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii